MELI YA URUSI YAZAMA BAHARI YA MEDITERANIA BAADA YA MLIPUKO MKUBWA

By Arushadigital

Meli ya mizigo inayomilikiwa na Urusi na iliyokuwa imebeba shehena kubwa ya gesi imezama katika Bahari ya Mediterania kati ya pwani za Libya na Malta baada ya kukumbwa na mlipuko mkubwa uliosababisha moto mkali, tukio lililozua taharuki na maswali kuhusu chanzo cha ajali hiyo.

Kwa mujibu wa maafisa wa mamlaka ya bandari nchini Libya, meli hiyo iliripotiwa kupata hitilafu ghafla baada ya kusikika kwa milipuko kadhaa kabla ya moto mkubwa kuzuka na kuanza kuiteketeza. Baadaye meli hiyo ilizama katika eneo hilo la bahari ambalo hutumiwa sana na meli za biashara na usafirishaji wa nishati.

Serikali ya Urusi imeituhumu Ukraine kwa kuhusika na tukio hilo, ikidai kuwa meli hiyo ilishambuliwa na ndege zisizo na rubani (drones) zilizodaiwa kurushwa kutoka katika pwani ya Libya. Hata hivyo, mamlaka za Ukraine hazijatoa kauli rasmi kuhusiana na tuhuma hizo hadi sasa.

Kwa upande wake, mamlaka ya bandari ya Libya imesema bado uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha mlipuko na moto uliosababisha kuzama kwa meli hiyo, ikieleza kuwa hakuna uthibitisho wa awali unaoonyesha kama tukio hilo lilitokana na shambulio au hitilafu ya kiufundi.

Mashuhuda waliokuwepo katika eneo hilo, akiwemo baadhi ya wavuvi na wakazi wa pwani ya Libya, wamesema meli hiyo ilionekana kubeba shehena kubwa ya gesi inayokadiriwa kufikia tani 62,000 kabla ya ajali hiyo kutokea.

Wizara ya Uchukuzi ya Urusi imethibitisha kuwa jumla ya mabaharia 30 raia wa Urusi walikuwa ndani ya meli hiyo wakati tukio hilo likitokea. Hata hivyo, juhudi za uokoaji zilizofanywa haraka na vikosi vya ulinzi vya Malta zimefanikiwa kuwaokoa wote wakiwa hai.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Malta, Byron Camilleri, amesema mabaharia hao walipatikana wakiwa ndani ya boti za uokoaji baada ya kuondoka kwenye meli hiyo wakati moto ulipoanza kuenea.

Amesema vikosi vya uokoaji vya jeshi la Malta vilifanya operesheni ya haraka katika eneo hilo la bahari na kuwahamisha mabaharia hao kwa usalama hadi katika eneo salama, huku baadhi yao wakipewa huduma za afya kutokana na mshtuko walioupata.

Tukio hilo limeongeza wasiwasi kuhusu usalama wa meli zinazopita katika Bahari ya Mediterania, hasa katika kipindi hiki ambacho mvutano wa kisiasa na kijeshi kati ya Urusi na Ukraine umeendelea kuathiri shughuli mbalimbali za kimataifa, ikiwemo usafirishaji wa nishati na bidhaa muhimu kupitia njia za baharini.

Wataalamu wa masuala ya usafirishaji wa baharini na usalama wanasema uchunguzi wa kina unahitajika kufanyika ili kubaini iwapo tukio hilo linahusiana na mgogoro wa kijeshi unaoendelea au ni ajali ya kawaida ya kiufundi inayoweza kutokea katika usafirishaji wa mizigo hatarishi kama gesi.