MWANAFUNZI DARAJA LA NNE AFARIKI AKISOMBWA NA MAJI AKIFUATA UFUNGUO WA DARASA ARUSHA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MWANAFUNZI wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Terati iliyopo Kata ya Murieti, Jijini Arusha, aitwaye Abdulrizaki Said, amefariki dunia baada ya kusombwa na maji ya mvua alipokuwa akijaribu kuvuka korongo lililokuwa limejaa maji mengi, wakati akitekeleza agizo la mwalimu wake la kwenda kuchukua ufunguo wa darasa.Taarifa za tukio hilo zinasema mwanafunzi huyo alikuwa ameagizwa na mwalimu wake kwenda kuchukua ufunguo wa darasa kwa mwanafunzi mwenzake ambaye hakuweza kufika shuleni siku hiyo kutokana na wazazi wake kumzuia kufuatia mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio Machi 5, 2026, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mashariki, Emmanuel Sanare, alisema mtoto huyo alikuwa tayari amefika shuleni kabla ya kupewa jukumu hilo na mwalimu wake.
“Mtoto huyu alifika shuleni asubuhi, lakini baada ya kufika akaagizwa na mwalimu kwenda kuchukua ufunguo kwa mwanafunzi mwenzake ambaye wazazi wake walimzuia kwenda shule kwa sababu ya mvua,” alisema Sanare.
Sanare alieleza kuwa wakati mwanafunzi huyo akielekea kutekeleza agizo hilo, alilazimika kuvuka korongo lililokuwa limejaa maji mengi ya mvua, ndipo mkasa huo ulipotokea na kusababisha kusombwa na maji hadi kupoteza maisha.
Aliongeza kuwa tatizo kubwa katika eneo hilo si tu kukosekana kwa vivuko salama kwa wanafunzi, bali pia kuchelewa kuanza kwa ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi Mashariki, ambayo ingeweza kupunguza umbali na hatari wanazokumbana nazo wanafunzi wanaolazimika kuvuka makorongo kufuata masomo katika Shule ya Msingi Terati.
Kwa mujibu wa Sanare, takribani asilimia 85 ya wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Msingi Terati wanatoka eneo la Mashariki, hali inayowalazimu kuvuka makorongo yenye maji hasa wakati wa mvua ili kufika shuleni.
“Ndiyo maana tulichukua hatua ya kutafuta eneo la kujenga shule ya Mashariki. Mkurugenzi wa Halmashauri alishatununulia eneo na hata tayari fedha za ujenzi zilishatengwa,” alifafanua.
Aliongeza kuwa kilichobaki kwa sasa ni kuanza kwa ujenzi huo, na kuiomba Halmashauri kupitia kwa Mkurugenzi kuhakikisha mkandarasi aliyepewa kazi hiyo anaanza ujenzi haraka ili kuondoa hatari inayowakabili wanafunzi.
“Tunachohitaji sasa ni Mkurugenzi kumsukuma mkandarasi aanze ujenzi wa shule haraka, kwa sababu wanafunzi wanazidi kuangamia kwa kulazimika kuvuka makorongo yenye maji mengi,” alisema Sanare.
Tukio hilo limeibua huzuni na maswali miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, hasa ikizingatiwa kuwa ndani ya kipindi cha wiki moja tu, wanafunzi wawili wa Shule ya Msingi Terati wameripotiwa kupoteza maisha baada ya kusombwa na maji wakati wakielekea au kurejea kutoka shuleni.
Wakazi wa eneo hilo wameendelea kuomba mamlaka husika kuchukua hatua za haraka ikiwemo ujenzi wa vivuko salama pamoja na kuharakisha ujenzi wa Shule ya Msingi Mashariki ili kuzuia matukio kama hayo kujirudia siku zijazo.
Ends...

0 Comments