WAHASIBU WATAKIWA KUIMARISHA UADILIFU NA WELEDI KATIKA USIMAMIZI WA FEDHA ZA UMMA

 WAHASIBU WATAKIWA KUIMARISHA UADILIFU NA WELEDI KATIKA USIMAMIZI WA FEDHA ZA UMMA

Na Ananngisye Mwateba | ARUSHA 

Wahasibu katika Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, nidhamu na kuzingatia kikamilifu misingi ya taaluma yao, kwa kuwa wao ni walinzi wakuu wa nidhamu na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.

Wito huo umetolewa jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wahasibu wa wizara hiyo na taasisi zake, ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Nkoba Mabula, akimwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, alisisitiza kuwa ubora wa taarifa za kifedha zinazotolewa na wahasibu una athari kubwa kwa uwajibikaji wa taasisi za serikali.

Alisema taarifa hizo pia huathiri taswira ya wizara mbele ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bunge pamoja na wananchi, ambao ndio wanufaika wakuu wa rasilimali za taifa.

“Wahasibu mnabeba dhamana kubwa ya kuhakikisha fedha za umma zinasimamiwa kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa. Ubora wa taarifa zenu za fedha una mchango mkubwa katika kujenga imani kwa taasisi za serikali,” alisema Mabula.

Aliongeza kuwa wizara hiyo imeendelea kusimamia vizuri matumizi ya fedha zake pamoja na taasisi zilizo chini yake, jambo lililoisaidia kupata hati safi kutoka kwa CAG kwa miaka mitatu mfululizo.

Kwa mujibu wa Mabula, mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wahasibu wanaofanya kazi katika wizara na taasisi zake.

Kutokana na hilo, aliwataka wahasibu hao kuendelea kudumisha uadilifu, weledi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ili kulinda mafanikio yaliyopatikana na kuimarisha zaidi mfumo wa usimamizi wa fedha za umma.

Aidha aliwahimiza kutumia kikao kazi hicho kama jukwaa muhimu la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga mshikamano wa kitaaluma, hatua ambayo itasaidia kuongeza ufanisi katika usimamizi wa fedha ndani ya wizara hiyo na taasisi zake.


Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, CPA Paul Kabale, alisema kikao kazi hicho kinalenga kuimarisha uwezo wa kitaaluma na kiutendaji wa wahasibu ili kuhakikisha majukumu ya kifedha katika wizara na taasisi zake yanatekelezwa kwa uwazi, uwajibikaji na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za fedha za umma.

Kabale alisema kupitia mafunzo hayo, wahasibu watapata fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali za kisasa za usimamizi wa fedha pamoja na kujadili changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Alimhakikishia Naibu Katibu Mkuu kuwa washiriki wa kikao hicho watatumia kikamilifu fursa ya mafunzo hayo na kwamba maarifa watakayopata yatasaidia kuboresha zaidi utendaji wao wa kila siku.

Kikao kazi hicho cha siku mbili kimewakutanisha wahasibu kutoka wizara hiyo na taasisi zake, huku kikihusisha wakufunzi mbalimbali kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Fedha pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Mbali na mada za kitaaluma kuhusu usimamizi wa fedha, washiriki pia wanatarajiwa kupata mafunzo mtambuka kuhusu afya ya akili yatakayotolewa na mtaalamu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ustawi wa watumishi katika utendaji wao wa kazi.











Post a Comment

0 Comments