MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU KUTOA HUKUMU YA KIHISTORIA KUHUSU UCHAGUZI MKUU WA TANZANIA 2020

 MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU KUTOA HUKUMU YA KIHISTORIA KUHUSU UCHAGUZI MKUU 2020

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

 

MAHAKAMA ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu yenye makao yake makuu jijini Arusha, inatarajiwa kutoa hukumu inayotajwa kuwa ya kihistoria kesho Ijumaa, Machi 6, 2026, katika kesi inayopinga uhalali wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2020.


Uamuzi huo unasubiriwa kwa shauku kubwa na wadau wa siasa, wanaharakati wa haki za binadamu na wachambuzi wa masuala ya kisheria ndani na nje ya Tanzania, kutokana na uzito wa hoja zilizowasilishwa mahakamani zikihusu madai ya ukiukwaji wa haki za kisiasa na kiraia wakati wa uchaguzi huo.


Kwa mujibu wa nyaraka za kesi hiyo, wadai waliwasilisha ushahidi mbalimbali kutoka kwa viongozi wa upinzani, wagombea na wapiga kura, wakidai kuwa kulikuwepo na vitendo vilivyokiuka haki za msingi za wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi, pamoja na madai ya matumizi ya nguvu, kukosekana kwa usawa wa kisiasa na vikwazo dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari.


Kesi hiyo ilifunguliwa mwezi Novemba mwaka 2020 na aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, marehemu Seif Sharif Hamad, aliyepinga kile alichodai kuwa ukiukwaji mkubwa wa sheria na kanuni za uchaguzi uliofanywa wakati wa mchakato wa uchaguzi huo.


Baada ya kifo chake mwezi Februari mwaka 2021, mahakama iliridhia Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, kuendeleza shauri hilo kama mwombaji mkuu kwa niaba ya wadai wengine.


Mbali na Shaibu, wadai wengine katika kesi hiyo ni wagombea wawili wa ubunge na Baraza la Wawakilishi pamoja na wapiga kura watatu walioandikishwa, ambao kwa pamoja wanadai kuwa haki zao za kisiasa na kiraia zilikiukwa katika mchakato mzima wa uchaguzi.


Katika hoja zao, wadai wanaomba mahakama itamke kuwa uchaguzi huo haukuzingatia misingi ya kidemokrasia na haki za binadamu, wakieleza kuwepo kwa vitendo mbalimbali vinavyodaiwa kuathiri uhalali wa matokeo ya uchaguzi huo. 


Miongoni mwa madai yaliyowasilishwa ni pamoja na kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea wa upinzani, madai ya kuwepo kwa kura zisizo halali, ukosefu wa uhuru wa tume ya uchaguzi, pamoja na vikwazo dhidi ya vyama vya siasa na vyombo vya habari wakati wa kipindi cha uchaguzi.


Aidha, wadai wameitaka mahakama kutoa maelekezo ya mageuzi ya kikatiba na kisheria ili kuimarisha mfumo wa uchaguzi nchini Tanzania na kuhakikisha kuwa uchaguzi wa baadaye unafanyika kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya demokrasia na haki za binadamu.


Kwa upande wa utetezi, Serikali ya Tanzania ilikanusha madai yote yaliyowasilishwa na wadai. Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya timu ya mawakili wa wadai, serikali ilichelewa kuwasilisha majibu yake mahakamani na ilipofanya hivyo ilikanusha tuhuma hizo bila kuwasilisha ushahidi wa kina unaounga mkono hoja zake.



Timu ya mawakili wa wadai inajumuisha wanasheria mashuhuri wa kimataifa akiwemo Fulgence Massawe wa Tanzania, Chidi Odinkalu wa Nigeria na Ibrahima Kane wa Senegal.


Kutokana na uzito wa kesi hiyo, mwaka 2025 mahakama iliruhusu taasisi kadhaa za kimataifa za haki za binadamu kuwasilisha maoni yao kama marafiki wa mahakama (amici curiae). 


Miongoni mwa taasisi hizo ni Robert F. Kennedy Human Rights, ambayo iliwasilisha uchambuzi kuhusu viwango vya kimataifa vya haki za kisiasa na uchaguzi huru na wa haki.



Wachambuzi wa masuala ya sheria na siasa wanasema hukumu hiyo inaweza kuwa na athari kubwa katika mjadala mpana wa mageuzi ya mfumo wa uchaguzi na demokrasia nchini Tanzania, huku ikitarajiwa pia kuweka alama muhimu katika historia ya maamuzi ya mahakama za kimataifa kuhusu haki za kisiasa barani Afrika.


Ends...

Post a Comment

0 Comments