SERIKALI YAIMARISHA KINGA YA JAMII, WANANCHI SEKTA ISIYO RASMI KUNUFAIKA ZAIDI
Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
SERIKALI imeahidi kuendelea kuimarisha mfumo wa kinga ya jamii nchini ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata ulinzi wa kiuchumi na kijamii, huku ikitangaza mafanikio makubwa ya ukuaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii na upanuzi wa huduma kwa sekta rasmi na isiyo rasmi.
Ahadi hiyo ilitolewa leo Februari 9,2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Clement Sangu, alipofungua Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Kinga ya Jamii na kuzindua rasmi Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya mwaka 2023 pamoja na Skimu ya Wananchi Waliojiajiri katika Sekta Isiyo Rasmi katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa AICC, jijini Arusha.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Sangu alisema mageuzi yaliyofanyika tangu mwaka 2018 yameimarisha uimara wa mifuko, kuongeza wanachama na kuboresha utoaji wa mafao kwa wakati.
“Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kisera na kisheria ili kila Mtanzania apate kinga dhidi ya majanga ya maisha kama uzee, maradhi, ulemavu na kupoteza kipato,” alisema Sangu.
Katika uzinduzi huo, Waziri Sangu pia alikabidhi vyeti vya utambuzi kwa wadau mbalimbali wa sekta ya kinga ya jamii waliotoa mchango mkubwa katika kuimarisha usalama mahala pa kazi pamoja na waajiri na wafanyakazi waliotunukiwa kwa uchangiaji bora katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Alisema hatua hiyo inalenga kuhamasisha uwajibikaji, nidhamu ya uchangiaji na utamaduni wa usalama kazini.
Waziri Sangu alisema idadi ya wanachama wa mifuko ya pensheni imeongezeka kwa kasi kutoka wanachama milioni 1.5 mwaka 2020 hadi milioni 3.1 mwaka 2025 — ongezeko la asilimia 106.
Mfuko wa NSSF umeongeza wanachama kutoka 808,935 hadi 2,213,659, huku PSSSF ukiongezeka kutoka 697,677 hadi 889,948 katika kipindi hicho.
Kwa mujibu wa Sangu, ukuaji huo umechangiwa na maboresho ya kisera, kuunganishwa kwa mifuko na upanuzi wa huduma kwa sekta isiyo rasmi.
Thamani ya uwekezaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii imeongezeka kutoka shilingi trilioni 10.43 mwaka 2020 hadi trilioni 24.20 kufikia Desemba 2025.
NSSF imeongeza thamani ya mfuko kutoka trilioni 4.36 hadi trilioni 10.40, huku PSSSF ikipanda kutoka trilioni 5.74 hadi trilioni 12.96.
Sangu alisema uimara huo umeongeza uwezo wa mifuko kulipa mafao kwa wakati, ambapo sasa wanachama hulipwa ndani ya siku 30 na pensheni hutolewa kila tarehe 25 ya mwezi.
Katika hatua ya kuboresha ustawi wa wastaafu, Serikali imeongeza kiwango cha chini cha pensheni kwa watumishi wa umma kutoka shilingi 100,000 hadi 250,000 kwa mwezi kuanzia Julai 2025.
Aidha, Serikali imeshalipa asilimia 95 ya deni la kihistoria la shilingi trilioni 4.46 la michango ya wanachama wa zamani wa PSSSF.
Waziri Sangu alizindua skimu maalum ya kinga ya jamii kwa wananchi waliojiajiri, ikilenga makundi ya wakulima, wavuvi, wachimbaji wadogo, mama lishe, bodaboda na wafanyabiashara wadogo.
Hadi Desemba 2025, wanachama 509,000 tayari wamejiunga, huku lengo likiwa kufikia zaidi ya wananchi milioni 5.5 ifikapo mwaka 2031.
“NSSF isimamie kikamilifu upanuzi wa skimu hii ili kuwafikia Watanzania walio wengi katika sekta isiyo rasmi,” alisisitiza.
Serikali pia imeendelea kuimarisha ustawi wa kaya maskini kupitia TASAF, ambapo zaidi ya kaya milioni 1.37 zenye watu milioni 5.5 zimenufaika na ruzuku ya zaidi ya shilingi trilioni 1.55 pamoja na ajira za muda kwa walengwa zaidi ya 600,000.
Waziri Sangu aliagiza bodi na menejimenti za mifuko kusimamia uwekezaji kwa tija na kuhakikisha waajiri wanawasilisha michango kwa wakati ili kulinda maslahi ya wanachama.
Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu sekta ya kinga ya jamii ili kuifanya kuwa nguzo ya ustawi wa wananchi na maendeleo ya uchumi wa taifa.
Ends











0 Comments