Na Joseph Ngilisho – ArushaDigital, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, leo Februari 9, 2026, ameibua hoja nzito mahakamani akilalamikia kucheleweshwa kwa mwenendo wa kesi inayomkabili, akisisitiza kuwa haki haipaswi kucheleweshwa kwa muda mrefu kiasi cha kumfanya mshitakiwa aendelee kubaki mahabusu bila usikilizwaji wa mara kwa mara.
Akiwasilisha hoja zake mbele ya majaji, Lissu amesema hadi sasa ametimiza siku 307 akiwa mahabusu, huku kesi yake ikisikilizwa kwa siku 15 pekee tangu kuanza kwake.
“Leo ni siku ya 307 tangu niwekwe mahabusu. Katika siku zote hizi, kesi hii imesikilizwa kwa siku 14 tu, na leo ni siku ya 15. Kuna siku 88 ambazo kesi haijasikilizwa kabisa tangu Novemba 12, 2025. Waheshimiwa majaji, haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa,” alisisitiza Lissu.
Lissu alirejea misingi ya kikatiba na kisheria inayoelekeza mahakama kuendesha mashauri ya jinai bila ucheleweshaji usio wa lazima, akieleza kuwa mwenendo wa sasa wa usikilizaji wa kesi kwa mfumo wa session katika Mahakama Kuu unachangia kucheleweshwa kwa haki.
“Katiba yetu, kupitia Ibara ya 107B, inaelekeza Mahakama kuendesha kesi bila kuchelewesha. Aidha, kifungu cha 5 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinaeleza wazi kuwa kesi zisikilizwe haraka. Kuendesha kesi kwa utaratibu wa session ndicho chanzo kikuu cha ucheleweshaji huu,” aliongeza.
Kauli hiyo imeibua mjadala mpana kuhusu ufanisi wa utaratibu wa usikilizwaji wa kesi katika Mahakama Kuu, huku wadau wa sheria wakisisitiza umuhimu wa kusawazisha taratibu za kimahakama na haki ya msingi ya mshitakiwa kusikilizwa kwa wakati.
Kesi hiyo inaendelea kufuatiliwa kwa karibu na wadau wa siasa na sheria nchini, ikitarajiwa kuendelea kusikilizwa kwa mujibu wa ratiba ya mahakama.
Ends..

0 Comments