THAMANI YA MFUKO NSSF YAPAA HADI TRILIONI 10.40,WAZIRI AITUNUKU NSSF CHETI KAMA MDAU MKUBWA WA USAJILI WA SKIMU HIFADHI YA WANANCHI WALIOJIAJIRI
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kuimarika kifedha huku thamani ya mfuko ikifikia shilingi trilioni 10.40 kufikia Desemba 2025, hatua inayoakisi uimara wa mfumo wa kinga ya jamii na uwezo wa mfuko kulipa mafao kwa wakati.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, katika Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Kinga ya Jamii uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC jijini Arusha, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Clement Sangu.
Mshomba alisema ukuaji huo unatokana na mageuzi ya kisera na kiutendaji yaliyoimarisha utendaji wa mfuko pamoja na kuupanua wigo wa huduma kwa wananchi wa sekta rasmi na isiyo rasmi.
Alibainisha kuwa ifikapo Juni 2026, michango ya wanachama inatarajiwa kufikia shilingi trilioni 2.99, huku mfuko ukiendelea kupata ziada ya zaidi ya shilingi trilioni moja kila mwaka, hali inayoonesha uimara wa kifedha na uendelevu wa mfuko katika kuhudumia wanachama wake.
“Upanuzi wa mifumo ya hifadhi na ushirikishwaji wa sekta isiyo rasmi ni msingi wa kujenga uchumi jumuishi unaomlinda kila Mtanzania,” alisema Mshomba.
Katika hatua ya kuimarisha ulinzi wa wananchi waliojiajiri, NSSF pia ilitunukiwa cheti cha usajili wa skimu mahususi ya hifadhi kwa wananchi wa sekta isiyo rasmi, hatua inayolenga kuwajumuisha zaidi Watanzania katika mfumo rasmi wa kinga ya jamii.
Akifungua mkutano huo, Waziri Sangu alieleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya kisera na kisheria ili kuhakikisha wananchi wote wanapata ulinzi wa kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, idadi ya wanachama wa mifuko ya pensheni imeongezeka kutoka milioni 1.5 mwaka 2020 hadi milioni 3.1 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 106. Ndani ya kipindi hicho, wanachama wa NSSF wameongezeka kutoka 808,935 hadi 2,213,659, huku PSSSF ikiongezeka kutoka 697,677 hadi 889,948.
Alisema thamani ya uwekezaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii imepanda kutoka shilingi trilioni 10.43 mwaka 2020 hadi trilioni 24.20 kufikia Desemba 2025. NSSF imeongeza thamani ya mfuko kutoka trilioni 4.36 hadi trilioni 10.40, huku PSSSF ikikua kutoka trilioni 5.74 hadi trilioni 12.96.
Waziri Sangu alisema maboresho hayo yameongeza ufanisi wa utoaji huduma ambapo wanachama hulipwa mafao ndani ya siku 30 na pensheni hulipwa kila tarehe 25 ya mwezi. Aidha, Serikali imeongeza kiwango cha chini cha pensheni kwa watumishi wa umma kutoka shilingi 100,000 hadi 250,000 kwa mwezi kuanzia Julai 2025.
Katika kutambua mchango wa wadau, Waziri Sangu aliitunuku NSSF cheti maalum cha heshima kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha mfumo wa kinga ya jamii, kuboresha usalama mahala pa kazi na kuendeleza uhimilivu wa kifedha wa wanachama.
Sambamba na hilo, alizindua rasmi Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya mwaka 2023 pamoja na skimu maalum ya hifadhi kwa wananchi waliojiajiri ikilenga wakulima, wavuvi, wachimbaji wadogo, mama lishe, bodaboda na wafanyabiashara wadogo.
Hadi Desemba 2025, zaidi ya wanachama 509,000 wamejiunga na skimu hiyo, huku lengo likiwa kuwafikia zaidi ya wananchi milioni 5.5 ifikapo mwaka 2031.
Serikali pia imeendelea kuimarisha ustawi wa kaya maskini kupitia TASAF ambapo zaidi ya kaya milioni 1.37 zenye watu milioni 5.5 zimenufaika na ruzuku ya zaidi ya shilingi trilioni 1.55 pamoja na ajira za muda kwa walengwa zaidi ya 600,000.
Waziri Sangu aliziagiza bodi na menejimenti za mifuko ya hifadhi ya jamii kusimamia uwekezaji kwa tija na kuhakikisha waajiri wanawasilisha michango kwa wakati ili kulinda maslahi ya wanachama.






0 Comments