GGM YANG’ARA SEKTA YA MADINI, YATUNUKIWA VYETI VIWILI KATIKA MKUTANO WA KINGA YA JAMII ARUSHA ,YAAHIDI KUENDELEA KUWA KINARA SEKTA YA MADINI

 GGM YANG’ARA SEKTA YA MADINI, YATUNUKIWA VYETI VIWILI KATIKA MKUTANO WA KINGA YA JAMII ARUSHA ,YAAHIDI KUENDELEA KUWA KINARA SEKTA YA MADINI

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

KAMPUNI ya uchimbaji madini ya Geita Gold Mining Limited (GGM) imetunukiwa vyeti viwili vya kutambua mchango wake katika usalama mahali pa kazi na utekelezaji bora wa hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi, katika mkutano wa wadau wa sekta ya kinga ya jamii uliofanyika AICC, Arusha


Vyeti hivyo vilikabidhiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deo Sangu, ikiwa ni sehemu ya utambuzi kwa taasisi zinazoongoza kwa kuzingatia sheria za kazi, usalama kazini na mchango wa kifedha kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo, Meneja Uwekezaji wa Uendelevu wa GGM, Gilbert Moriya, alisema kampuni hiyo imeendelea kuwa kielelezo cha uongozi bora na uwajibikaji katika sekta ya madini.


“Sisi ni vinara katika sekta ya madini, hilo halina ubishi. Tunawafanyakazi zaidi ya 7,000 na tunahakikisha kila mmoja anafanya kazi kwa kufuata sheria na kanuni za kazi. Ndiyo maana leo tumetunukiwa vyeti viwili,” alisema Moriya.


Aliongeza kuwa tuzo ya kwanza kutoka WCF inatambua juhudi za GGM katika kuhakikisha usalama kazini, huku cheti cha pili kutoka NSSF kikitambua utii wa kampuni katika kulipa michango ya hifadhi ya jamii kwa wakati.


“Vyeti hivi vinaonesha wazi kuwa mgodi wetu unazingatia kikamilifu sheria, kanuni na viwango vya usalama pamoja na hifadhi ya jamii. Tutaendelea kuishi tunu zetu kuu—usalama, uwajibikaji na uendelevu—ili kubaki kinara katika sekta ya madini nchini na kimataifa,” alisisitiza Moriya.


Mkutano huo uliowakutanisha wadau mbalimbali wa kinga ya jamii pia uliashiria jinsi waajiri wanaotekeleza wajibu wao kikamilifu wanavyotambuliwa, huku thamani ya mfuko wa NSSF ikifikia trilioni 10.40 na michango ya wanachama ikitarajiwa kufikia trilioni 2.99 ifikapo Juni 2026, hatua inayodhihirisha ukuaji wa mifumo ya kinga ya jamii nchini.




ENDS..

Post a Comment

0 Comments