WACHIMBAJI WATAMBULIWA RASMI, WAZIRI SANGU AWATUNUKU FEMATA CHETI AICC

WACHIMBAJI WATAMBULIWA RASMI, WAZIRI SANGU AWATUNUKU FEMATA CHETI AICC

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA


SERIKALI imeendelea kutambua mchango wa wachimbaji nchini baada ya Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Tanzania (FEMATA) kutunukiwa cheti maalum cha kutambua mchango wake katika sekta ya kinga ya jamii, katika hafla iliyoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi), Mhe. Deus Clement Sangu.

Tuzo hiyo ilitolewa leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya kinga ya jamii ulioenda sambamba na uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii na skimu ya usajili kwa wananchi waliojiajiri.

Akizungumza baada ya kupokea cheti hicho, Mwenyekiti wa Wachimbaji Mkoa wa Manyara, Elisha Nelson Mnyawi, aliyemwakilisha Rais wa FEMATA, Mhe. Johny Wambura, alisema kutambuliwa kwa wachimbaji ni ishara ya mchango mkubwa wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa na ustawi wa jamii.

Alisema wachimbaji wameendelea kuwa wadau muhimu katika mifuko ya hifadhi ya jamii huku mchango wao ukiendelea kukua sambamba na juhudi za serikali za kupanua wigo wa kinga ya jamii kwa wananchi wote, hususan wale waliojiajiri.

“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii na tunatoa shukrani kwa serikali pamoja na NSSF kwa kutambua mchango wa wachimbaji katika maendeleo ya nchi. Cheti hiki ni heshima kubwa kwa wachimbaji wote nchini na kinathibitisha kuwa mchango wetu unatambulika na kuthaminiwa,” alisema Mnyawi.

Katika hafla hiyo, Waziri Sangu alisisitiza dhamira ya serikali ya kuimarisha mfumo wa kinga ya jamii ili kuhakikisha wananchi wote, wakiwemo sekta isiyo rasmi kama wachimbaji, wanapata ulinzi wa kijamii kuanzia ajira hadi uzeeni.

Uzinduzi wa skimu ya usajili kwa wananchi waliojiajiri unaotarajiwa kupanua wigo wa wanufaika wa hifadhi ya jamii ulienda sambamba na hatua ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutunukiwa cheti cha usajili wa skimu maalum ya hifadhi kwa kundi hilo.

Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, alisema thamani ya mfuko imeendelea kuimarika na kufikia shilingi trilioni 10.40 huku michango ya wanachama ikitarajiwa kufikia trilioni 2.99 ifikapo Juni 2026. Aliongeza kuwa mfuko umekuwa ukipata ziada ya zaidi ya shilingi trilioni moja kila mwaka, jambo linalodhihirisha uimara wa sekta ya hifadhi ya jamii nchini.

Serikali imeeleza kuwa ushiriki wa sekta kama wachimbaji katika mifuko ya hifadhi ya jamii ni nguzo muhimu ya kujenga mfumo jumuishi wa kinga ya jamii unaolenga kulinda kipato, ajira na ustawi wa wananchi .




Ends...

Post a Comment

0 Comments