SERIKALI YAONYA WATUMISHI WA UMMA MATUMIZI YA MIFUMO ISIYO RASMI,YASISITIZA NIDHAMU YA KIDIGITALI KULINDA USALAMA WA TAARIFA ZA UMMA

 Na Joseph Ngilisho — ARUSHA 

SERIKALI imewataka watumishi wa umma kuachana na matumizi ya mifumo isiyo rasmi katika mawasiliano na utekelezaji wa majukumu ya kikazi, ikisisitiza matumizi ya mifumo rasmi ya Serikali Mtandao kama nguzo ya kulinda usalama wa taarifa za umma na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa leo February 19,2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, wakati akifunga Kikao Kazi cha Sita cha Serikali Mtandao (eGA) kilichofanyika kwa siku tatu katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), na kukutanisha takribani washiriki 1,000 kutoka sekta za umma na binafsi.


Akisisitiza nidhamu ya kidijitali, Waziri Kikwete alionya matumizi ya barua pepe binafsi kama Gmail, Yahoo na Hotmail katika mawasiliano ya kikazi, akibainisha kuwa mifumo rasmi ya serikali ndiyo yenye viwango vinavyohitajika kulinda nyaraka na taarifa nyeti za umma. 


Alisema pia baadhi ya watumishi bado wanatumia njia zisizo rasmi katika miamala na mikopo, jambo linalosababisha hatari za kifedha na kiutumishi licha ya kuwepo kwa mifumo salama ya serikali.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Benedict Ndomba, alisema maazimio ya kikao hicho yatatekelezwa kwa ushirikiano wa wadau wote ili kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ubora wa huduma za umma.


Alieleza kuwa kikao hicho kimejadili kwa kina mada 14 kuhusu utekelezaji wa miradi ya TEHAMA serikalini, kikiweka mkazo katika:

kuunganisha mifumo ya taasisi za umma,

kuimarisha ulinzi dhidi ya mashambulizi ya kimtandao,

na kuharakisha utoaji wa huduma kupitia majukwaa ya kidijitali.

Kwa mujibu wa Ndomba, serikali mtandao ni kichocheo cha uchumi wa kidijitali, kinachopunguza urasimu na kuongeza kasi ya huduma kama malipo ya serikali na usimamizi wa rasilimali watu.


 Katika hafla hiyo, eGA ilikabidhi tuzo kwa taasisi zilizozingatia sheria, kanuni na viwango vya utekelezaji wa miradi ya TEHAMA.


Kwa niaba ya Bunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro, alisema mageuzi ya serikali mtandao yamepunguza gharama za uendeshaji na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi. 


Alitolea mfano Bunge kuondoa matumizi ya karatasi na kuhamia mifumo ya kielektroniki, hatua iliyoleta ufanisi mkubwa wa kiutendaji.


Ndumbaro alisisitiza umuhimu wa kuunganisha mifumo ya serikali ili mwananchi apate huduma kwa kutumia namba moja ya utambulisho wa taifa, huku Bunge likiahidi kuendelea kuunga mkono marekebisho ya kisheria na kibajeti yanayohitajika kuharakisha mchakato huo.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Toba Nguvilla, alisema kuendelea kwa Arusha kuwa mwenyeji wa mikutano ya Serikali Mtandao ni ishara ya imani ya taifa kwa mchango wa mkoa huo katika mageuzi ya kidijitali.


 Alihimiza taasisi za umma kuzingatia kikamilifu sera na viwango vya TEHAMA ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.


Serikali imeagiza waajiri katika taasisi za umma kuwekeza zaidi katika mafunzo ya wataalamu wa TEHAMA ndani na nje ya nchi, ili kukabiliana na mabadiliko ya haraka ya teknolojia na kuimarisha kinga dhidi ya vitisho vya kimtandao. 


Aidha, imehimiza ushirikiano wa karibu kati ya serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kujenga mfumo salama na jumuishi wa huduma za umma.


Katika kuhitimisha, viongozi wa mkutano huo walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono na uongozi katika kusukuma mageuzi ya kidijitali, wakibainisha kuwa hatua hizo zimeongeza kasi ya utoaji huduma na kuimarisha uwajibikaji serikalini.







ENDS...

Post a Comment

0 Comments