MFANYABIASHARA MAARUFU WA MADINI ARUSHA 'BANJOO'AUAWA KINYAMA MWILI WAOKOTWA KONDOA UKIWA UMEHARIBIKA, ATOBOLEWA MACHO

 KIFO CHA MFANYABIASHARA WA MADINI “BANJOO” CHAZUA MASWALI, MWILI WAPATIKANA KONDOA

Na Joseph Ngilisho — Arusha


Mfanyabiashara Maarufu wa madini, Abdilah Musa maarufu kama Banjoo, mkazi wa Sanawari jijini Arusha, amepatikana amefariki dunia baada ya kuripotiwa kupotea kwa siku kadhaa. Mwili wake uligunduliwa katika eneo la Bereko, wilayani Kondoa mkoani Dodoma, ukiwa umeharibika vibaya.

Kwa mujibu wa mtoto wake, Mussa Abdilah, familia ilipigiwa simu na wananchi waliodai kuona mwili wa mtu usiotambulika kando ya barabara eneo la Bereko. Baada ya kufika eneo la tukio, ndugu walithibitisha kuwa mwili huo ni wa baba yao.

Mussa amesema mwili huo ulikuwa na majeraha makubwa, ikiwemo kuondolewa macho na kuvunjwa mkono—hali inayozidisha utata wa mazingira ya kifo hicho.

Akieleza mlolongo wa matukio kabla ya kifo hicho, Mussa amesema kuwa Februari 12, 2026, Banjoo aliondoka nyumbani kuelekea mazoezini (gym) katika jengo la Ngorongoro jijini Arusha. Hata hivyo, taarifa za awali zinaeleza kuwa watu wasiojulikana walifika eneo hilo na kumchukua, kabla ya kutoweka naye. Jitihada za familia na ndugu kumtafuta hazikuzaa matunda hadi walipopokea taarifa za kupatikana kwa mwili wake Kondoa.

Tukio hilo limeacha simanzi na maswali mengi kwa familia na wakazi wa Arusha, huku mamlaka za uchunguzi zikitarajiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu chanzo cha kifo na watuhumiwa wanaohusishwa.

Taarifa zaidi zitaendelea kutolewa kadri uchunguzi unavyoendelea.

Ends..

Post a Comment

0 Comments