MPYA YA MFANYABIASHARA WA MADINI BANJOO MWILI WAOKOTWA KONDOA UKIWA UMETOBOLEWA MACHO NA KUVUNJWA MKONO, MENGI YAZUNGUMZWA MSIBANI

Mwili wa Mfanyabiashara wa Madini “Banjoo” Umepatikana Umetobolewa Macho na Kuvunjwa Mkono Kondoa

Na Joseph Ngilisho – KONDOA

KONDOA, Dodoma – Mwili wa mfanyabiashara wa madini, Abdilah Mussa, maarufu kama Banjoo, umepatikana umetupwa katika msitu wa Hifadhi ya Salanga, Kijiji cha Masawi, wilayani Kondoa, ukiwa umeharibika kwa kiasi kikubwa huku macho yake yakiwa yametobolewa na mkono mmoja kuvunjwa.

Tukio hili limetokea baada ya Banjoo kutoweka siku ya Februari 12, wakati alipokuwa eneo la Jengo la Ngorongoro akiwa kwenye mazoezi ya Jim, ambapo watu wasiojulikana walimchukua na kuondoka naye. Taarifa za kupotea kwake zilitolewa na ndugu zake jana, zikithibitisha kuwa kwa siku sita Banjoo hakuwa ameonekana.

Ally Abdi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Masawi, amesema kuwa kuna mtu mmoja aliyedai kuiona maiti hiyo siku ya Jumamosi na kujaribu kuripoti kijijini, lakini wananchi walidhani kuwa mtu huyo alikuwa na tatizo la akili. Hata hivyo, siku ya Jumapili, mtu huyo akarudia kauli hiyo, ndipo wananchi walipochukua pikipiki na kwenda eneo la tukio, ambapo walikuta mwili wa marehemu pembezoni mwa barabara.

Mwenyekiti Abdi ameongeza kuwa msitu huo ni eneo lililo mbali zaidi ya kilomita mbili kutoka barabara kuu, hivyo mara nyingi watu hawapiti sana katika eneo hilo, jambo linalofanya matukio ya aina hii kuwa hatari zaidi. Aidha, amebainisha kuwa mwili huu ni wa tatu kuonekana katika msitu huo, jambo linaloongeza hofu na wasiwasi miongoni mwa wananchi.

Wakazi wa eneo hilo wameleana vikali unyama huu, wakisema kuwa unyama wa kumuuwa mtu kutoka mbali na kisha kutupwa msituni ni jambo linalowatia mashaka makubwa na kuashiria uwepo wa uhalifu wa kigaidi au wa kikundi cha kigaidi. Wanakadiria kuwa ulinzi wa maeneo ya mbali kama msitu wa Salanga unahitaji kuimarishwa ili kuzuia matukio kama haya kutokea tena.

Hadi sasa, Jeshi la Polisi wilaya ya Kondoa limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio hili, huku wakidai kuwa watakaobainika kufanya uhalifu huu watafikishwa mbele ya sheria, huku wananchi wakiwa na hofu na wasiwasi kutokana na unyama na uhalifu wa namna hii uliotokea.

 






Ends..

Post a Comment

0 Comments