Waziri Mkuu Aagiza Kufukuzwa Kazi Daktari Aliyemdhulumu Mgonjwa Tabora
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, ameagiza kuchukuliwa hatua kali ikiwemo kufutwa kazi kwa daktari mmoja wa Hospitali ya Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, anayetuhumiwa kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 18 aliyekuwa akipatiwa matibabu ya tatizo la uzazi.
Dk. Mwigulu alitoa agizo hilo akiwa eneo la Leganga, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua maeneo yaliyoathiriwa na vurugu za Oktoba 29, mwaka huu.
Alichosema Waziri Mkuu
Akieleza tukio hilo kwa masikitiko makubwa, Dk. Mwigulu alisema daktari huyo alimchoma mgonjwa sindano ya usingizi kisha akamtendea unyama huo huku nesi pamoja na wataalamu wengine wakiwa mashahidi wa tukio.
“Mgonjwa alikwenda na mume wake, daktari akamsikiliza, akamdanganya kwa kumchoma sindano ya usingizi na ndipo akamdhulumu kijinsia. Mgonjwa alipozinduka, tayari alikuwa amebakwa. Haya ni mambo ya hovyo sana,” alisema Dk. Mwigulu.
Amesema ushahidi uliotolewa na muuguzi na baadhi ya madaktari wengine unathibitisha kwamba tukio hilo lilitokea wakiwa kazini.
Hatua Zinazochukuliwa
Dk. Mwigulu aliagiza mara moja daktari huyo kufutiwa leseni, kufikishwa kwenye vyombo vya dola na kuchukuliwa hatua kali bila kusamihiana.
“Huyu akamatwe na asiachiwe. Nimeelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais afukuzwe kazi mara moja,” alisisitiza.
Waziri Mkuu amesema serikali haitavumilia vitendo vya udhalilishaji vinavyofanywa na watu waliokabidhiwa jukumu la kulinda maisha ya wananchi.
Ends..

0 Comments