Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
ALIYEKUWA Meya wa Jiji la Arusha na Diwani mteule wa Kata ya Kaloleni, Maxmillian Iranghe (kulia), ameibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha kuwania tena nafasi ya Umeya wa Jiji la Arusha baada ya kuwashinda wagombea wenzake, Matuyani Laizer na Credo Kifukwe.
Katika uchaguzi huo uliofanyika ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Iranghe alipata kura 19, akifuatiwa na Matuyani Laizer aliyepata kura 14, huku Credo Kifukwe akiambulia kura 3.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Iranghe aliwashukuru wajumbe kwa imani waliomwonesha na kuahidi kuendeleza kazi aliyoiita “kazi iliyotukuka” kwa manufaa ya wakazi wa Jiji la Arusha.
Iranghe alisema awamu yake mpya ya uongozi itaweka mkazo katika kuunganisha madiwani wote bila kujali tofauti za kiitikadi ili kufanikisha maendeleo ya jiji.
Kipaumbele chake kikubwa ni kuboresha miundombinu ya barabara, hasa zile za vumbi katika kata na mitaa yote 154 ya jiji. Aliahidi kuweka vifusi, kujenga mitaro ya maji taka na kuhakikisha barabara zinapitika kipindi chote cha mwaka.
> “Changamoto ya barabara sasa imepata mwarobaini,” alisema Meya Iranghe.
Aidha, aliahidi kusimamia kwa karibu utekelezaji wa ahadi ya ujenzi wa hoteli 50 za hadhi ya nyota tano katika kipindi cha miaka mitano, mradi ulioasisiwa na Mbunge wa Arusha, Paul Makonda, kama sehemu ya kuongeza uwekezaji na ajira.
Katika uchaguzi huo huo, nafasi ya Naibu Meya iliangukia kwa Julius Ole Sekeyani, Diwani wa Kata ya Terat, aliyeshinda kwa kura 22 dhidi ya Amitana Troule aliyepata kura 16.
Meya mteule, Naibu Meya na madiwani wanatarajiwa kupigiwa kura ili kudhinishwa na baadaye kuapishwa rasmi Desemba 4, 2025, katika kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani la Jiji la Arusha,kufuatiwa baraza hilo kuwa na diwani wa chama kimoja cha upinzani ambaye kwa haki ya kawaida hataweza kubadilisha matokeo hayo.
-ends...


















0 Comments