KISHILI ANGUKIA PUA MERU ,LUCAS KAAYA ACHAGULIWA KWA KISHINDO MCHAKATO WA MWENYEKITI WA HALMASHAURI

 Na Joseph Ngilisho, ARUSHA

MERU: ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meru, Jeremiah Kishili ameshindwa kutetea nafasi yake baada ya kushindwa katika uchaguzi wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo, ambapo Lucas Essaya Kaaya, Diwani wa Kata ya King'ori, aliibuka mshindi.

Kaaya alipata kura 21, huku Kishili akipata kura 15 katika mchakato huo uliohusisha madiwani wateule wa Baraza la Madiwani wa CCM ndani ya halmashauri hiyo.

Mara baada ya kutangazwa mshindi, Kaaya aliahidi kuongoza chombo hicho kwa weledi na kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Alisema halmashauri hiyo itatenga asilimia 40 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara katika kata zote, ikiwemo ujenzi wa mifereji na uwekaji wa vifusi.

“Nina kiu kubwa ya kutatua changamoto za wananchi wa Meru. Zipo kata hazina maji, sehemu nyingine umeme bado ni changamoto. Tunakwenda kuibadilisha Meru. Pia tutashirikiana na Mbunge Joshua Nassari ili kuhakikisha tunapata angalau kilomita 30 za lami,” alisema Kaaya.


Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meru, Husna Maganga aliibuka mshindi kwa kupata kura 28, akimshinda Leah Mbise aliyepata kura 7.

Akizungumza baada ya ushindi, Husna aliahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na Baraza la Madiwani pamoja na watendaji wa halmashauri hiyo ili kuongeza kasi ya maendeleo.

“Tunahitaji kuongeza nguvu kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani kupitia vyanzo vyetu mbalimbali. Nikishirikiana na madiwani wenzangu, tutahakikisha halmashauri inafanya maboresho makubwa kwa manufaa ya wananchi wa Meru,” alisema.

Baadhi ya madiwani wa ccm,Julius Mungure na Abrahamu Kaaya waliohojiwa walidai wanaimani na viongozi hao wakidai ni wasomi wabobezi hivyo ni mwanzo mzuri wa kwenda kuisuka Meru Mpya.




Ends



Post a Comment

0 Comments