VIONGOZI WA MILA NA DINI MERU, WALAANI MAANDAMANO, WAMWOMBEA BARAKA MBUNGE NASARI ,AFUNGUKA MAZITO AKATAA KUWA MBUNGE WA HARAMBEE

 Na Joseph Ngilisho – Arumeru


VIONGOZI wa mila, dini na wanasiasa wilayani Arumeru wamefanya maombi maalumu ya kulaani vurugu na umwagaji damu uliotokea katika maandamano kufuatia uchaguzi wa Oktoba 29, huku wakitoa onyo kali kwa wananchi—hasa vijana—kujiepusha na maandamano hayo wanayoyaita “chanzo cha machafuko na kurudisha nyuma maendeleo.”


Mkutano huo ulifanyika leo Dc 6,2025 katika Mti maarufu wa jadi wa Mringaringa, uliopo Kata ya Poli, ambapo Mshiri Mkuu wa jadi ya Wameru, Willson Mbise, alitoa tamko zito akisisitiza kuwa jamii ya Wameru haitasita kuwachukulia hatua wale wote watakaohamasisha au kushiriki maandamano.

> “Atakayethubutu kurudia kitendo cha maandamano tutamchukulia hatua,” alisema kwa msisitizo.


Mbise aliwaonya vijana kutokubali kutumiwa au kudanganywa na watu wenye malengo binafsi, akibainisha kuwa maandamano hayajawahi kuleta maendeleo bali huzua majeraha na uhasama unaowagawa wananchi.

>

“Sasa nyinyi Wameru mnadanganywa ili mjikaange wenyewe. Mimi nawaomba kama kiongozi wenu msikubali. Vita haina maendeleo,” alisema Mbise.



Katika mkusanyiko huo, viongozi wa mila walifanya maombi maalumu kwa ajili ya Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, wakimtaka Mungu ampe hekima, uadilifu na moyo wa kuwatumikia wananchi bila upendeleo.


Akizungumza katika Mkutano huo, Nasari aliwashukuru wananchi kwa kumuamini na kumchagua, akiahidi kuongoza kwa misingi ya maendeleo na uwajibikaji wa kweli.

>

“Mimi ni mbunge wa maendeleo. Sitaki kuwa mbunge wa kutatua shida za mtu mmoja mmoja,” alisema.

 

Alionya tabia ya baadhi ya watu kumualika katika makundi ya michango ya harusi, kwaya na sherehe mbalimbali, akisisitiza kwamba jukumu lake kubwa ni kuleta maendeleo ya pamoja na kushughulikia kero za wananchi wa Meru.

Akirejea tukio la vurugu lililotokea majuzi, Nasari alisema limekumbusha wajibu mkubwa ulio mbele yao kama viongozi.

> “Awamu hii, kwa sisi mliotuchagua, tutawafanya muone maendeleo ambayo hamjawahi kuyaona,” aliahidi.


Katika hatua nyingine, aliwaita madiwani wa jimbo hilo mbele ya wazee wa mila ambapo waliombewa na kukabidhiwa jukumu la kutekeleza majukumu yao kwa bidii na uadilifu.

>

“Uongozi wetu huu, na mimi nikiwa nimepewa fimbo ya kuwaongoza, nitahakikisha tunawajibika kweli kweli—usiku na mchana—kuwatumikia wananchi,” alisema.


Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa dini, wazee wa mila, madiwani na mamia ya wananchi wa koo mbalimbali za jamii ya  wameru, ikiwa ni ishara ya umoja katika kulinda amani, mshikamano na kuhamasisha maendeleo ya jimbo hilo.

Naye  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meru, Lucas Kaaya, amesema anazitambua vyema changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo na kuwataka waendelee kuwa na imani na viongozi wao wanaoahidi kuzitatua katika kata zote.

Akizungumza katika mkutano huo Kaaya alisema kuwa kwa ushirikiano wa karibu kati yake, Mbunge wa jimbo na Baraza la Madiwani, watahakikisha wanatembelea kata zote ili kujionea changamoto zilizopo na kusimamia utekelezaji wa maazimio na mahitaji ambayo madiwani wamekuwa wakiyasemea.

Aliongeza kuwa uongozi huo umejipanga kuhakikisha kuwa kila kata inapata ufumbuzi wa changamoto zake kwa wakati, huku akiwataka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu wakati juhudi za kutatua matatizo yao zikiendelea.

Aidha, Kaaya aliahidi kuendeleza ushirikiano na viongozi wa mila katika kuhakikisha jamii inapata maendeleo, utulivu na mshikamano unaohitajika kwa ustawi wa Halmashauri ya Meru.












Ends...

Post a Comment

0 Comments