Franone Mining Yang’ara Mirerani, Waziri Mavunde Aipongeza kwa Uwekezaji Mkubwa wa Huduma za Jamii
Na Joseph Ngilisho, MIRERANI
SEKTA ya madini nchini imeendelea kupata sura mpya baada ya Kampuni ya Franone Mining Ltd kutikisa Mirerani kwa hatua yake ya kipekee ya kuwekeza katika huduma muhimu za kijamii ndani ya machimbo ya Tanzanite—hatua iliyowavutia wachimbaji na kuiweka kampuni hiyo kwenye ramani nzuri kwa wadau wenye dhamira ya kweli ya kuwainua Watanzania.
Akizungumza katika mkutano uliohusisha wadau wa madini Mirerani, Waziri wa Madini, Anthony Peter Mavunde, aliisifu na kuipigia mfano Franone Mining kwa kuwa mstari wa mbele kutoa huduma zinazobeba uhai na ustawi wa jamii ya wachimbaji.
> “Franone Mining imeonyesha moyo wa kipekee. Ujenzi wa zahanati katikati ya machimbo ya Tanzanite ni jambo kubwa linaloonyesha uongozi makini, uzalendo na dira ya kujali watu. Ni jambo tunalolipongeza kwa nguvu zote,” alisema Waziri Mavunde.
Zahanati ya Kwanza Ndani ya Machimbo—Tumaini Jipya kwa Wachimbaji
Kwa mara ya kwanza katika historia ya eneo hilo, Franone imejitolea kujenga zahanati kamili ndani ya machimbo, itakayotoa huduma za afya kwa maelfu ya wachimbaji wa Tanzanite wanaoishi na kufanya shughuli zao ndani ya eneo hatarishi, mara nyingi bila huduma za haraka za tiba.
Zahanati hiyo itakuwa mkombozi hasa wakati wa dharura kama ajali, majeraha ya kazi, uchovu wa kupumua ndani ya mashimo, na magonjwa mengine yanayowakumba wachimbaji.
Kampuni Yaonyesha Moyo Mkubwa—Yatenga Milioni 10 kwa Tomarini ya Kijani
Katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Franone Mining Ltd, Onesmo Mbise, alitikisa hadhira baada ya kutangaza kuchangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati nyingine katika machimbo ya Tomarini ya Kijani, eneo la Lemshuku kata ya Komolo.
Mbise alisema mchango huo ni sehemu ya shukrani zake kwa eneo lililomlea.
> “Mheshimiwa Waziri, mimi ni mtoto wa hapa Lemshuku. Nimeona ni wajibu wangu kurudisha kwa jamii. Hiyo ndiyo sababu nimejitolea milioni 10 kuhakikisha zahanati hii inasimama na inatoa huduma bora,” alisema kwa uthabiti.
Wachimbaji waliopata nafasi ya kuzungumza walimpongeza Mbise wakisema kitendo hicho kinaweka alama ya kudumu kwa jamii ya wachimbaji ambao muda mrefu wameishi katikati ya changamoto nyingi za kiafya.
God Charity Naye Yatinga Kwenye Orodha ya Wafadhili – Yajitolea Kisima cha Maji
Sambamba na Franone, taasisi ya God Charity chini ya Mkurugenzi God Mwanga imejitolea kisima cha maji kitakachowanufaisha wachimbaji walio katika maeneo yenye uhaba wa maji safi na salama.
Waziri Mavunde aliipongeza taasisi hiyo akisema ushirikiano wa wadau kama hao unaipa sekta ya madini sura ya matumaini mapya.
> “Moyo mliouonyesha—Franone na God Charity—unaijenga Mirerani mpya. Serikali inatambua, inathamini na inakaribisha wadau wote wenye mtazamo wa kuinua jamii,” alisema Waziri.
Mirerani Yafunguka—Wadau Wahimiza Kampuni Nyingine Kuiga Mfano
Ufadhili huu wa kimkakati umeibua gumzo Mirerani, wadau wakihimiza kampuni nyingine kuiga mfano huu wa Franone katika kuinua maisha ya wachimbaji wanaochangia pato kubwa la taifa kupitia Tanzanite.
Wakizungumza baada ya mkutano huo, baadhi ya wachimbaji walisema ujenzi wa zahanati na upatikanaji wa maji vitapunguza gharama, kuokoa muda na kulinda usalama wa afya zao.
-ends-


0 Comments