Na Joseph Ngilisho-ARUMERU
Viongozi wa dini, wazee wa mila wa kabila la Wameru (Washili) na viongozi mbalimbali wa koo wa jamii ya wameru zaidi ya 500 wameungana katika maombi maalum ya kuwaombea Watanzania waliopoteza maisha au kuumia katika vurugu za uchaguzi zilizotokea Oktoba 29, 2025.
Ibada hiyo imefanyika leo desemba 06,2025 chini ya Mti wa Mringaringa uliopo kata ya Poli na kufuatiwa na mvua kubwa, mmoja wa miti maarufu na yenye historia ya kimila wilayani Arumeru, ambapo kawaida hutumika kwa matambiko, baraka na sala za kijamii kwa jamii ya Wameru.
Kusanyiko hilo limeandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Samwel Nasary, ikiwa ni sehemu ya shukrani zake kwa wananchi wa jimbo hilo kwa kumchagua kuwaongoza. Mbunge Nasary alisisitiza kuwa shukrani za kweli hazionyeshwi kwa maneno tu, bali pia kwa kuwaongoza wananchi katika shughuli za kujenga amani na kuimarisha umoja wa kitaifa.
Katika hotuba yake, alieleza kuwa anataka kuanza utumishi wake wa ubunge kwa kusimama pamoja na wananchi katika maombi, akiamini kuwa taifa linahitaji uponyaji na utulivu baada ya yaliyotokea wakati wa uchaguzi.
Kusanyiko hilo pia limehudhuriwa na madiwani mbalimbali wa kata za Jimbo la Arumeru Mashariki, ambao walishiriki katika sala, dua na baraka zinazolenga kuombea faraja kwa familia zilizoguswa na vurugu hizo pamoja na kudumisha amani nchini.
Viongozi wa dini kutoka madhehebu tofauti waliongoza sala za kuombea maridhiano, mshikamano na upendo miongoni mwa Watanzania. Wazee wa mila wa Washili nao walitoa baraka za kimila, wakisisitiza umuhimu wa kulinda misingi ya amani ambayo imekuwa uti wa mgongo wa jamii ya Meru kwa vizazi vingi.
Wito wa Amani na Maridhiano
Katika ujumbe wao wa pamoja, viongozi hao waliitaka serikali, vyama vya siasa na wananchi wote kutanguliza uzalendo, hekima na maelewano ili kuhakikisha matukio kama ya Oktoba 29 hayajirudii tena nchini. Walihimiza Watanzania kuendelea kuwa mabalozi wa amani katika maeneo yao na kuendelea kuombea taifa.
Kusanyiko hilo limehitimishwa kwa sala za baraka chini ya Mti wa Mringaringa, zikionyesha mshikamano wa kipekee kati ya viongozi wa dini, wazee wa mila, viongozi wa kisiasa na jamii kwa ujumla.
Ends..














0 Comments