TUME YA UCHUNGUZI YAWAHAKIKISHIA WATANZANIA KUTOKUWA NA LONGOLONGO ITAMHOJI YEYOTE BILA KUPEPESA MACHO

TUME YA UCHUNGUZI YAHAKIKISHA UHURU NA UWELEDI KATIKA KAZI YAKE

Na Joseph Ngilisho – DAR ES SALAAM


Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani baada ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Mohamed Othman Chande, amesema tume hiyo itafanya kazi yake kwa weledi, uwazi na uhuru bila kuingiliwa na mtu yeyote.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jaji Chande alisema tume imejipanga kufanya uchunguzi wa kina unaoendana na matarajio ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa, kwa kuzingatia kuwa kazi hiyo inafuatiliwa kwa karibu ndani na nje ya nchi.


“Tumebaini kuwa watu wanataka uchunguzi kamili, usifanyike nusunusu. Wanataka uwazi, na ushahidi utakaopokelewa uwe wenye nguvu na unaoweza kutumika kisheria,” alisema Jaji Chande.


Hadidu za Rejea

Amebainisha kuwa tume imetengewa maeneo sita ya msingi yatakayopigiwa kazi, ikiwemo:


Kuchunguza na kubaini chanzo halisi cha matukio ya uvunjifu wa amani.

Kubaini malengo na waliopanga kutekeleza vitendo hivyo.

Kutathmini madhara yaliyotokea kama vifo, majeruhi, uharibifu wa mali na hasara za kiuchumi.

Kuchambua mazingira na hatua zilizochukuliwa na serikali na vyombo vyake.

Kupendekeza maeneo yanayohitaji kuimarishwa ili kuongeza uwajibikaji na kulinda usalama, utawala bora, na haki za binadamu.

Kutengeneza mfumo madhubuti wa majadiliano ya kisiasa na kijamii ili kuzuia kurudiwa kwa vurugu.

Ameongeza kuwa tume pia imepewa uwanja mpana kuchunguza jambo lolote itakaloona linahusiana na majukumu yake bila kuhitaji kibali cha ziada.


Mwenendo wa Kimahakama

Jaji Chande amesema tume itafanya kazi kwa taratibu zenye mwelekeo wa kimahakama, ambapo mashahidi wataapa kabla ya kutoa ushahidi ili taarifa zao ziweze kutumika ipasavyo.


Amesema licha ya tume kuwa na mamlaka ya kutoa wito na hata kushurutisha ushirikiano inapobidi, haitatumia nguvu bali inatarajia ushirikiano wa hiari kutoka kwa wananchi na wadau.


Mbinu za Utekelezaji

Katika kutekeleza majukumu yake, tume itatumia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na:


Mapitio na uchambuzi wa nyaraka;

Mahojiano ya ana kwa ana na kwa njia ya mtandao;

Dodoso na baruapepe;

Barua za kawaida;

Kutembelea maeneo husika;

Ushauri wa kitaalamu;

Mijadala ya makundi mbalimbali;

Kupokea taarifa kupitia simu na ujumbe mfupi.

Kwa mujibu wa Jaji Chande, hatua hizi zote zitahakikisha matokeo ya uchunguzi yanakuwa ya kuaminika, yenye uhalisia na yatakayosaidia taifa kuimarisha misingi ya amani na maridhiano ya kitaifa.


Post a Comment

0 Comments