TAHADHARI YA KUTOWEKA KWA PUNDA YATOLEWA: BIASHARA HARAMU YA UVUKAJI MIPAKA YATISHIA UHAI WAO
CHAMA cha Ustawi wa Wanyama Tanzania (ASPA) kimetoa tahadhari nzito juu ya hatari ya kutoweka kwa punda nchini, kutokana na biashara haramu ya kuwasafirisha kinyemela kwenda nchi jirani kwa ajili ya kuchunwa ngozi.
Tahadhari hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki jijini Arusha na Afisa Elimu ya Ustawi wa Wanyama wa ASPA, Diana Msemo, katika mafunzo kwa wanahabari yaliyoandaliwa kuhamasisha uzingatiaji wa haki na ustawi wa wanyama.
Msemo amesema kuwa ongezeko la mahitaji ya ngozi za punda katika soko la kimataifa limechochea kuimarika kwa mtandao wa biashara haramu, hali inayosababisha kupungua kwa kasi kwa idadi ya punda nchini.
> “Punda ni kundi la pili kwa umuhimu katika mifugo nchini, baada ya ng’ombe. Wanachangia pakubwa katika uchumi na maisha ya jamii za wafugaji. Lakini sasa mahitaji ya ngozi zao yamefungua mlango wa biashara haramu, hususan katika nchi jirani kama Kenya ambako wanachinjwa kwa siri,” alisema.
Kwa mujibu wa Msemo, punda wengi wanasafirishwa kupitia njia zisizotambuliwa na mamlaka, na kufikishwa katika minyororo ya biashara ya ngozi ambako hawana ulinzi wa kisheria.
Ameeleza kuwa punda ni nguzo muhimu katika shughuli za kilimo, usafirishaji wa mizigo na majukumu ya nyumbani, na kuwaangamiza kunawaathiri zaidi watoto wa jamii za wafugaji wanaotegemea wanyama hao kuwezesha majukumu ya kila siku na kuwafanya waweze kuhudhuria masomo bila vikwazo.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa ASPA, Albert Mbwambo, amesema jamii inapaswa kutambua umuhimu wa punda na wajibu wa kuwalinda.
> “Pamoja na kupungua kwa kasi kwa idadi ya punda, bado tunapaswa kuendelea kuielimisha jamii kuhusu madhara ya biashara hii haramu. Ni lazima tuhakikishe wanyama hawa wanadumishwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.
ASPA kwa kushirikiana na wadau wake akiwemo BROOKE East Africa, inaendelea kufanya kampeni za kuhamasisha ustawi wa wanyama na kuelimisha wananchi kuhusu athari za biashara ya punda na umuhimu wa kuilinda rasilimali hiyo muhimu.
Ends..








0 Comments