WADAU WA ELIMU ARUSHA WAIBUA MIKAKATI MIPYA KUKUZA UFAULU 2026

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA


Wadau wa elimu mkoani Arusha wamekubaliana kutekeleza mpango mkakati mpya na maazimio ya sekta ya elimu kwa mwaka wa masomo 2026, ikiwa ni matokeo ya tathmini ya utekelezaji wa mwaka 2025.


Kikao kazi hicho kimefanyika jana katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kimewakutanisha viongozi wa elimu, wataalamu na wadau kutoka sekta ya umma na binafsi kwa lengo la kuweka mwelekeo mpya wa kuinua kiwango cha ufaulu katika mkoa huo.

Akiwasilisha taarifa ya tathmini hiyo, Katibu Tawala Msaidizi wa Idara ya Elimu, Mwl. Vicent Kyombo, alisema kikao hicho kinatoa fursa kwa wadau kubadilishana uzoefu, kutathmini changamoto zilizopo na kupanga kwa pamoja mbinu za kuzitatua.


Alisema kuwa mpango wa mwaka 2026 umejengwa katika msingi wa ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja ili kuhakikisha maendeleo ya elimu yanakwenda sambamba na mahitaji ya jamii ya sasa.

Mwl. Kyombo alitaja maeneo muhimu ya kipaumbele kuwa,Kuimarisha uongozi na usimamizi kwa kuwa na viongozi wabunifu na makini katika shule na ngazi za halmashauri,Kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi ili kuongeza ari ya kufundisha na kujifunza


Kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji kulingana na mabadiliko ya mitaala na teknolojia,Kuhakikisha uwepo wa chakula cha mchana shuleni ili kupunguza utoro na kuongeza umakini darasani,Kukuza michezo, sanaa, vipaji na ukakamavu wa wanafunzi kama sehemu ya malezi jumuishi.


“Hata hivyo, idara ya elimu itaendelea kuimarisha mpango huu shirikishi utakaojumuisha wadau wote wa sekta ya elimu ili kupata maono ya pamoja, kukabili changamoto kwa umoja na hatimaye kuongeza kiwango cha ufaulu kwenye mitihani ya ndani na kitaifa,” alisema Mwl. Kyombo.

Kaulimbiu ya kikao kazi hicho ni,“Elimu Bora ni Msingi wa Maendeleo Endelevu – Kila Mdau Mkoa wa Arusha Awajibike.”






-ends...

Post a Comment

0 Comments