RAIS SAMIA: MATUKIO YA OKTOBA 29 HAYAKUWA MAANDAMANO BALI NI VURUGU ZILIZOPANGWA
Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
DAR ES SALAAM — Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema tukio la Oktoba 29, 2025 halikuwa maandamano halali kama ilivyodaiwa, bali ni vurugu zilizoandaliwa kwa nia mahsusi ya kuvuruga amani na kuathiri mali za wananchi na Serikali.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mkutano maalum na Wazee wa mkoa huo, Rais Samia alisema kiwango cha uharibifu kilichotokea hakilingani kamwe na tabia ya maandamano ya kawaida yanayotambuliwa na Katiba.
“Takwimu zinazoletwa sasa zinaonyesha majengo kadhaa ya Serikali yamechomwa moto, miradi ya wananchi imeharibiwa, vituo vya mafuta, magari ya Serikali, biashara binafsi na vituo vingi vya Polisi vimeunguzwa. Sasa tujiulize, hayo ni maandamano au vurugu?” alisema Rais Samia.
Alifafanua kuwa maandamano halali huandaliwa kwa utaratibu na kwa lengo la kuwasilisha maoni ya wananchi, bila kushambulia mali za umma au kuvamia maeneo ya usalama.
“Katika kituo cha Polisi unakwenda kufanya nini? Hilo ni jaribio la kupata silaha. Madhumuni ya kuwa na silaha mkononi ni nini? Haya hayakuwa maandamano — zilikuwa vurugu zilizoandaliwa kwa makusudi,” alisisitiza.
Rais Samia alitetea hatua zilizochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama, akisema matumizi ya nguvu yalikuwa sawia na ukubwa wa tukio.
“Serikali ina wajibu wa kulinda mipaka ya nchi na usalama wa raia na mali zao. Tunapoambiwa tumetumia nguvu kubwa, tujiulize: nguvu ndogo ingekuwa ipi? Tuwatazame waliokuwa wamejiandaa kufanya mapinduzi hadi wafanikiwe? Hapo patakuwa na dola kweli?” alihoji.
Aliongeza kuwa si Tanzania pekee yenye kuchukua hatua kali wakati wa vurugu, bali hata mataifa mengine duniani hufanya hivyo kulinda uthabiti wa kiusalama.
“Wengine wanaotulaumu kuwa tulitumia nguvu kubwa, walitaka nini? Tuache mob ifanye kile walichoelekezwa na kufadhiliwa? Hapana. Tuliapa kuilinda nchi na usalama wa raia wake, na tutafanya hivyo bila kutetereka,” alisema.
Rais Samia aliwataka Watanzania kuendelea kulinda amani na kukataa kutumiwa na watu wanaotaka kuvuruga nchi kupitia vurugu zinazoitwa maandamano.
-ends.....

0 Comments