BARAZA JIPYA H/SHAURI YA ARUSHA MOTO KASI YA MWENYEKITI WA HALMASHAURI USIPIME AAHIDI MAGEUZI MAKUBWA YA KIUCHUMI ,KUPAISHA MAPATO HADI BIL.10

Baraza Jipya Arumeru Latoa Ahadi za Mageuzi; Mapato Kuongezeka, Barabara na Umeme Kipelekwa Kipaumbele

Na Joseph Ngilisho, Arumeru


MWENYEKITI Mpya wa Halmashauri ya Arusha Wilaya ya Arumeru, Baraka Simon, amewataka wananchi wa Halmashauri hiyo kutembea kifua mbele akisisitiza kuwa baraza jipya la madiwani limejipanga kuwaletea maendeleo ya kasi na viwango vya juu katika kipindi kijacho.


Akihutubia Baraza la Madiwani leo Dec 2,2025 mara baada ya kuchaguliwa kwa kishindo, Simon alisema uongozi wake umejipanga kuongeza mapato ya halmashauri kutoka Sh bilioni 6.9 za sasa hadi kufikia Sh bilioni 10 katika kipindi cha miaka mitano.

Akitaja vipaumbele vyake, alisema halmashauri itaanza na maboresho ya miundombinu, hasa barabara korofi zinazowapa wananchi adha katika maeneo mbalimbali.

> “Halmashauri yetu inakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara. Mimi pamoja na madiwani, tukishirikiana na Tanroads na Tarura, tutahakikisha tunafuta machozi ya wananchi kwa kuboresha barabara zote ili ziweze kupitika muda wote, hususan wakati wa masika,” alisema Simon.


Aidha, alisisitiza kuwa atasimamia kwa karibu misingi ya utawala bora kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji, kata hadi idara za halmashauri ili kuhakikisha wananchi wanasikilizwa na kuhudumiwa ipasavyo. Vilevile, atashirikia na na REA kuhakikisha vijiji vyenye uhaba wa umeme vinapata huduma hiyo kwa wakati.

Kuhusu mikopo na ajira, Simon alisema uongozi wake utaweka kipaumbele katika kuwawezesha vijana na wanawake kuchangamkia fursa za kiuchumi kupitia mifuko ya uwezeshaji.

Mafunzo kwa Madiwani Wapya

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo aliitaka menejimenti ya Halmashauri kuhakikisha inatoa semina na mafunzo kwa madiwani mapema iwezekanavyo, ili kuwaongezea uelewa na ufanisi wa kazi, hasa kwa madiwani wapya walioteuliwa kwa mara ya kwanza.

> “Ni muhimu madiwani wote wapatiwe mafunzo ya utendaji, usimamizi wa miradi na misingi ya kisheria ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na tija kwa wananchi,” alisisitiza.


Madiwani waunga Mkono Ari ya Mageuzi


Diwani wa Kata ya Kisongo, Violet Ngowo, alimpongeza mwenyekiti huyo na kuahidi ushirikiano, akisisitiza kuwa watafuatilia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya maji katika kata hiyo ili wananchi wapate huduma ya uhakika.

> “Kisongo tumepitia changamoto ya maji kwa muda mrefu. Tuko tayari kusimamia miradi yote hadi ikamilike kwa maslahi ya wananchi,” alisema Ngowo.


Naye Diwani wa Kata ya Olorien, Hendry Aikoi, alisema baraza hilo lina ari mpya ya kufanya kazi kwa uadilifu na kasi kubwa.

> “Wananchi wanatarajia mengi kutoka kwetu. Tutahakikisha miradi ya miundombinu na huduma za jamii inatekelezwa na kukamilika kwa wakati,” alisema Aikoi.


Simon aliwataka madiwani wote kuwa wamoja na kuweka mbele maslahi ya wananchi ili kufanikisha maendeleo endelevu ndani ya Wilaya ya Arumeru.






Ends..

Post a Comment

0 Comments