RC SENDIGA AIPIGA PINI BAR MAARUFU YA BARAZANI BABATI,INATIRIRISHA VINYESI BARAA

Joseph Ngilisho- Arushadigital – BABATI 

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, ameifungia  bar maarufu ya Barazani iliyopo mjini Babati, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza na kubaini kuwepo kwa mtiririko wa maji machafu yenye kinyesi cha binadamu unaotoka katika eneo hilo na kusambaa kwenye makazi ya wananchi, hali iliyosababisha madhara ya kiafya na mazingira.


Katika ziara hiyo, Sendiga amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Babati kwa kushirikiana na OCD wa Wilaya hiyo, kuifunga mara moja bar hiyo hadi mmiliki wake atakapojisalimisha binafsi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kutoa maelezo na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.


Mkuu wa Mkoa amesema tatizo hilo limekuwa kero kubwa kwa wananchi wanaoishi jirani na eneo hilo, akieleza kuwa maji taka hayo yamesababisha harufu kali, kuathiri usafi wa mazingira, na kuongeza hatari ya magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu, homa ya matumbo na maambukizi ya ngozi, hususan kwa watoto na wazee. Ameeleza kuwa Serikali haiwezi kuvumilia vitendo vinavyohatarisha afya ya wananchi na kudhalilisha haki yao ya kuishi katika mazingira safi na salama.


Kwa mujibu wa taarifa, wananchi waliathirika walilazimika kupiga simu moja kwa moja kwa Mkuu wa Mkoa baada ya kudai kuwa kero yao haikupata ufumbuzi kupitia mamlaka za chini, licha ya malalamiko ya mara kwa mara. Hatua hiyo ilichochea ziara ya dharura ya Mkuu wa Mkoa ili kujionea hali halisi na kuchukua maamuzi ya haraka.


Awali, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji Babati ameeleza kuwa mmiliki wa eneo hilo amekuwa akikaidi maagizo ya Halmashauri ya kuhakikisha usafi wa mazingira, ikiwemo kurekebisha mifumo ya maji taka, licha ya kupewa taarifa na maelekezo mara kadhaa.


Mhe. Sendiga ametoa onyo kali kwa wamiliki wa biashara na makazi yote mkoani Manyara kuzingatia sheria za usafi wa mazingira, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kukiuka taratibu na kuhatarisha afya ya wananchi. Ameagiza pia viongozi wa ngazi za chini kuongeza ufuatiliaji na uwajibikaji ili kero za wananchi zipatiwe ufumbuzi kwa wakati bila kusubiri kuingiliwa na uongozi wa juu.


Wananchi wanaoishi jirani na bar hiyo wamesema mtiririko wa maji taka yenye kinyesi cha binadamu umekuwa ukipita karibu na makazi yao kwa muda mrefu, hali iliyosababisha harufu kali isiyovumilika na kuharibu kabisa mazingira ya eneo hilo. Wameeleza kuwa wakati wa jioni na usiku, harufu huongezeka na kufanya maisha kuwa magumu, hadi wengine kushindwa kufungua madirisha au kula chakula kwa amani.


Wakazi hao wamedai kuwa maji hayo yamekuwa yakisambaa hadi kwenye njia zinazotumiwa na watoto kwenda shule na maeneo ya kuchezea, jambo lililoongeza hofu ya maambukizi ya magonjwa ya mlipuko. Baadhi yao wamesema watoto wamekuwa wakilalamikia maumivu ya tumbo na matatizo ya ngozi, hali wanayoihusisha moja kwa moja na uchafu huo unaozunguka makazi yao.


Wananchi pia wamelalamikia kuporomoka kwa heshima na hadhi ya makazi yao, wakieleza kuwa wageni wamekuwa wakikwepa kufika katika eneo hilo kutokana na harufu na uchafu, jambo lililoathiri hata shughuli zao ndogondogo za kiuchumi. Wamesisitiza kuwa hali hiyo imekuwa ikiwafanya waishi katika mazingira yasiyo ya kibinadamu, kinyume na haki ya msingi ya kuishi katika mazingira safi na salama.


Aidha, wananchi hao wamesema walitoa taarifa mara kadhaa kwa viongozi wa ngazi za mtaa na kata bila kupata msaada wa haraka, jambo lililowalazimu kuwasiliana moja kwa moja na Mkuu wa Mkoa. Wamepongeza hatua iliyochukuliwa na Mhe. Queen Sendiga, wakisema imewarejeshea matumaini na imani kuwa Serikali inawasikiliza na iko tayari kulinda afya na ustawi wa wananchi wake.


Ends..

Post a Comment

0 Comments