MARAIS WATATU WA EAC WAKOSA MKUTANO WA 25 ARUSHA LEO/MARCH 7,2026!

 MARAIS WATATU WA EAC WAKOSA MKUTANO WA 25 ARUSHA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA 

MARAIS watatu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hawajashiriki katika Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wa jumuiya hiyo unaofanyika leo Machi 7, 2026, jijini Arusha, hali inayozua mjadala kuhusu ajenda muhimu zinazotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo wa ngazi ya juu.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Veronica Nduva, amethibitisha kuwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame; Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Félix Tshisekedi; pamoja na Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, wameomba radhi kutohudhuria mkutano huo na badala yake kuwatuma mawaziri kuwawakilisha.

Kutokuwepo kwa viongozi hao kunawaacha marais watano pekee waliothibitisha kuhudhuria mkutano huo muhimu wa kikanda. Waliothibitisha kushiriki ni Rais wa Kenya na Mwenyekiti wa sasa wa EAC, William Ruto; Rais wa Tanzania ambaye pia ni mwenyeji wa mkutano huo, Samia Suluhu Hassan; Rais wa Uganda, Yoweri Museveni; Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye; pamoja na Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud.

Licha ya kukosekana kwa baadhi ya wakuu wa nchi, mkutano huo unaendelea kupewa uzito mkubwa kutokana na ajenda nzito za kiuchumi na kisera zinazotarajiwa kujadiliwa. Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na gazeti la The East African, viongozi wa EAC wanatarajiwa kuzindua mfumo mmoja wa dhamana ya forodha utakaorahisisha biashara ndani ya ukanda huo.

Mfumo huo mpya unalenga kuondoa changamoto iliyokuwa ikiwasumbua wafanyabiashara kulazimika kulipia dhamana nyingi wanaposafirisha mizigo kupitia mipaka mbalimbali ya nchi wanachama. Kupitia mfumo huo wa pamoja, wafanyabiashara watalipa dhamana mara moja tu, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza kasi ya biashara ya kikanda.

Aidha, mkutano huo unatarajiwa kuzindua Mkakati wa Saba wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa jumuiya hiyo, ambao utaweka dira ya ukuaji wa uchumi, kuimarisha mtangamano wa kikanda na kuongeza ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Viongozi hao pia wanatarajiwa kujadili uteuzi wa Katibu Mkuu mpya wa EAC pamoja na majaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki, taasisi muhimu inayosimamia tafsiri na utekelezaji wa sheria za jumuiya hiyo.

Mbali na masuala ya uchumi na uongozi, mkutano huo pia unatarajiwa kujadili kwa kina hali ya usalama katika ukanda wa Afrika Mashariki. Hii ni kutokana na changamoto za migogoro zinazoendelea katika baadhi ya nchi wanachama, hususan katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na Sudan Kusini.

Sudan Kusini bado inakabiliwa na migogoro ya ndani ya kisiasa na kiusalama, huku hali ya uhusiano kati ya Rwanda na DRC ikiendelea kuwa tete kutokana na tuhuma za pande mbili kuhusu kuhusika katika machafuko yanayoendelea mashariki mwa DRC.

Kutokana na hali hiyo, wachambuzi wa siasa za kikanda wanaona mkutano huo wa Arusha kuwa na umuhimu mkubwa katika kutafuta mwelekeo mpya wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kiusalama ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Post a Comment

0 Comments