SHEIKH HARUNA LOTTA HUSSEIN ATEULIWA KATIBU MKUU TWARIQA TAIFA
....Uteuzi watangazwa kwenye futari kubwa Arusha; aahidi mageuzi, miradi ya kujitegemea na kuimarisha umoja wa Waislamu.
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
TAASISI kongwe ya dini ya Kiislamu ya Twariqa Tanzania imeingia katika ukurasa mpya wa uongozi baada ya kumteua rasmi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, Sheikh Haruna Lotta Husein, kuwa Katibu Mkuu wa Twariqa Taifa, akichukua nafasi ya uongozi katika kipindi kinachotarajiwa kuleta mageuzi na kuimarisha misingi ya maendeleo ya taasisi hiyo.
Uteuzi huo ulitangazwa hadharani March 5,2026 katika hafla kubwa ya futari iliyofanyika Zawia Kuu ya Arusha, tukio lililowakutanisha mamia ya waumini wa Kiislamu kutoka mikoa mbalimbali nchini waliokusanyika kusherehekea mwezi mtukufu wa Ramadhani, kuimarisha mshikamano wa kiimani na kumuenzi aliyekuwa kiongozi mashuhuri wa taasisi hiyo, marehemu Salimu Daruwesshi, maarufu kama “Mti Mkavu.”
Hafla hiyo ilifanyika katika mazingira ya ibada, dua na mshikamano wa hali ya juu, ambapo waumini walishiriki futari ya pamoja, kufanya dua na kuombea amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Katika mkesha maalumu wa dua uliofanyika wakati wa tukio hilo, waumini walimuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na taifa kwa ujumla ili liendelee kudumisha amani, utulivu na mshikamano miongoni mwa wananchi.
AAHIDI UONGOZI WA USHIRIKIANO
Akizungumza mara baada ya kutangazwa kushika nafasi hiyo nyeti, Sheikh Haruna Lotta Husein alitoa shukrani kwa viongozi na wanachama wa taasisi hiyo kwa kumuamini na kumpa dhamana hiyo kubwa ya kuiongoza taasisi katika ngazi ya taifa.
Alisema nafasi hiyo ni jukumu zito linalohitaji ushirikiano wa pamoja kutoka kwa viongozi, wanachama na jamii ya Kiislamu kwa ujumla ili kuhakikisha malengo ya taasisi yanafikiwa.
“Ni heshima kubwa kwangu kupewa dhamana hii. Ninaahidi kufungua milango ya mashauriano na ushirikiano kwa Waislamu wote ili kuhakikisha Twariqa inaendelea kutimiza wajibu wake wa kiroho na kijamii kwa manufaa ya jamii nzima,” alisema Sheikh Haruna.
Alisisitiza kuwa katika kipindi chake cha uongozi ataweka mkazo mkubwa katika kuimarisha miradi ya maendeleo endelevu itakayoiwezesha taasisi hiyo kujitegemea kiuchumi.
Kwa mujibu wake, taasisi nyingi za kijamii na kidini zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya kutegemea misaada kutoka kwa wahisani, hali ambayo inaweza kupunguzwa kwa kubuni miradi ya kiuchumi itakayosaidia kuendesha shughuli za taasisi kwa uhuru zaidi.
“Tutahakikisha tunaanzisha na kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ili taasisi iweze kujitegemea badala ya kutegemea wahisani pekee,” alisisitiza.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kudumisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Waislamu, huku akiishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuliongoza taifa kwa hekima na busara.
VIONGOZI WAPYA WATANGAZWA
Mbali na uteuzi wa Katibu Mkuu, hafla hiyo pia ilishuhudia utangazaji wa viongozi mbalimbali katika ngazi tofauti ndani ya taasisi hiyo, hatua inayolenga kuimarisha mfumo wa uongozi na kuongeza uwazi katika usimamizi wa shughuli za Twariqa Taifa.
Awali, Sheikh Halfa Jafar Fundi Haji kutoka Mkoa wa Kilimanjaro ndiye aliyetangaza rasmi viongozi hao wapya na kuwataka kutumikia taasisi kwa moyo wa kujitolea, uadilifu na mshikamano.
Akizungumza mbele ya viongozi na wanachama wa taasisi hiyo, Sheikh Halfa Jafar alisema uteuzi huo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uongozi na kusukuma mbele malengo ya taasisi hiyo katika nyanja za kiroho na kijamii.
Alieleza kuwa viongozi walioteuliwa kuanzia ngazi ya Naibu Sheikh, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wanapaswa kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha taasisi inaendeshwa kwa misingi ya uwazi, uwajibikaji na umoja.
“Tunawashukuru viongozi wote waliokubali dhamana hii. Tunaamini wataitumikia taasisi kwa moyo wa kujitolea na kuhakikisha shughuli zake zinaendelea kwa mafanikio,” alisema Sheikh Halfa Jafar.
UMOJA WA WANACHAMA WAONGEZWA NGUVU
Katika mkutano huo, viongozi pia waliwashukuru wanachama wa makundi mbalimbali ya Twariqa ambao wameendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiimani za taasisi hiyo, ikiwemo harambee na mipango ya maendeleo.
Kwa mujibu wa viongozi hao, ushirikiano uliopo miongoni mwa wanachama umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa taasisi hiyo na kuongeza mshikamano ndani ya jamii ya waumini.
Washiriki wa mkutano huo pia walipata fursa ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya taasisi pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano ili kuendeleza shughuli zake katika siku zijazo.
MATARAJIO MAPYA KWA TWARIQA TAIFA
Sheikh Halfa Jafar Fundi Haji aliwataka viongozi wapya kuweka mbele maslahi ya taasisi na kuhakikisha wanadumisha umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama.
Mwisho wa hafla hiyo, aliwashukuru waumini kwa mshikamano wao pamoja na waandishi wa habari kwa kufika na kuripoti tukio hilo.
Kwa ujumla, tukio hilo limeonekana kuwa ishara ya mwanzo wa awamu mpya ya uongozi ndani ya Twariqa Tanzania, huku waumini wakieleza matumaini kuwa uongozi mpya utaimarisha zaidi shughuli za kiroho, kijamii na maendeleo ya taasisi hiyo katika miaka ijayo.
Ends..



0 Comments