WATU SITA WAHOFIWA KUPOTEZA MAISHA BAADA YA GARI KUSOMBWA NA MAFURIKO NGORONGORO

 Na Joseph Ngilisho | NGORONGORO


HOFU na simanzi zimetanda miongoni mwa wakazi wa Kata ya Malambo, wilayani Ngorongoro, baada ya watu sita kuhisiwa kupoteza maisha kufuatia gari dogo kusombwa na maji makubwa ya mafuriko wakati likijaribu kuvuka Mto Sanjan jioni ya Machi 6, 2026.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea majira ya jioni wakati gari hilo lilipokuwa likitokea mnadani Mbugani kuelekea Kijiji cha Malambo, katika Kata ya Malambo, likiwa limebeba abiria kadhaa waliokuwa wakirejea makwao baada ya shughuli za mnada.

Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo, gari hilo lilikuwa limebeba jumla ya watu tisa akiwemo dereva ambaye pia anadaiwa kuwa mmiliki wa gari hilo. 

Inadaiwa kuwa wakati dereva akijaribu kulivusha gari katika mto huo, maji ya mafuriko yaliyokuwa yakitiririka kwa kasi kubwa yalilisukuma na kulisomba gari hilo.

Katika juhudi za haraka za uokoaji zilizofanywa na wananchi waliokuwa karibu na eneo la tukio, watu watatu walifanikiwa kuokolewa wakiwa hai jioni ya siku hiyo. 

Hata hivyo, hadi sasa miili ya watu wanne tayari imepatikana, huku watu wawili wakiendelea kutafutwa baada ya kupotea katika mkasa huo.

Wananchi wa maeneo ya jirani kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji wanaendelea na zoezi la kutafuta miili ya watu hao wawili ambao bado hawajapatikana. 

Hata hivyo, kutokana na nguvu ya maji na muda uliopita tangu kutokea kwa tukio hilo, matumaini ya kuwapata wakiwa hai yanaelezwa kuwa madogo.

Akizungumzia tukio hilo, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Mheshimiwa Yanick Ndoinyo, ametoa salamu za pole kwa wakazi wa Kijiji cha Malambo pamoja na familia zilizopoteza ndugu na jamaa zao katika ajali hiyo.

Mbunge huyo aliwataka wananchi kuwa waangalifu zaidi wanapovuka mito hususan katika kipindi hiki cha mvua nyingi, akisisitiza kuwa tahadhari ni muhimu ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

“Tunaomboleza pamoja na familia zilizopoteza wapendwa wao. Ni muhimu wananchi wetu wakachukua tahadhari kubwa wanapovuka mito wakati wa mvua, kwa sababu maji ya mafuriko yanaweza kuongezeka ghafla na kusababisha majanga kama haya,” alisema.

Tukio hilo limeibua huzuni kubwa katika jamii ya wakazi wa Malambo na maeneo ya jirani, huku wengi wakikusanyika karibu na eneo la mto kufuatilia maendeleo ya zoezi la utafutaji linaloendelea hadi sasa.

NB:picha ya Mtandao, haihusiani  na story hii

Ends..

Post a Comment

0 Comments