WAZIRI MKUU MWIGULU NCHEMBA AKUBALI OMBI LA MBUNGE WA MONDULI KUHIFADHI ENEO LA MALISHO NA MAFUNZO YA KIJESHI
Na Joseph Ngilisho | MONDULI
Mbunge wa Jimbo la Monduli, Joseph Isack, amewasilisha ombi la wananchi wa wilaya hiyo kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, la kutaka eneo lililotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo na mafunzo ya kijeshi kuendelea kubaki kwa matumizi hayo kwa manufaa ya wananchi na usalama wa taifa.
Mbunge huyo aliwasilisha ombi hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Monduli mbele ya Waziri Mkuu, ambapo alieleza kuwa eneo hilo lina umuhimu mkubwa kwa jamii ya wafugaji pamoja na kwa mafunzo ya majeshi ya ulinzi na usalama.
Katika hotuba yake, Mbunge Isack alisema wananchi wa Monduli wanathamini uwepo wa eneo hilo na wanapenda liendelee kutumika kwa malengo yake ya awali ya malisho ya mifugo na mafunzo ya kijeshi.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa niaba ya wananchi wa Monduli tunaomba eneo hili liendelee kubaki kwa matumizi ya malisho na mafunzo ya kijeshi. Ni eneo lenye umuhimu mkubwa kwa wananchi wetu wanaotegemea mifugo pamoja na kwa usalama wa taifa,” alisema.
Mbunge huyo aliongeza kuwa baadhi ya watu wameanza kujenga nyumba za kudumu ndani ya eneo hilo, hali ambayo inaweza kuathiri matumizi yaliyokusudiwa ya ardhi hiyo.
Kutokana na hali hiyo, aliomba serikali kulinda eneo hilo na kuhakikisha halibadilishwi matumizi yake, huku akisisitiza kuwa wananchi hawaoni sababu ya serikali kulipa fidia kwa watu waliojenga nyumba za kudumu katika eneo hilo.
Akijibu ombi hilo, Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba alikubali ombi la Mbunge huyo na wananchi wa Monduli, akisema serikali imeamua kuendelea kulihifadhi eneo hilo kwa matumizi ya malisho ya mifugo na mafunzo ya kijeshi kwa maslahi mapana ya taifa na wananchi.
Alisema tayari amewasiliana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kufikia makubaliano ya kuendeleza ushirikiano kati ya wananchi na jeshi katika matumizi ya eneo hilo.
“Serikali imekubali ombi hili. Tayari nimewasiliana na Mkuu wa Majeshi wa JWTZ na tumekubaliana kuwa eneo hili liendelee kubaki kwa matumizi ya malisho na mafunzo ya kijeshi kwa manufaa ya wananchi wa Monduli na kwa maslahi mapana ya nchi yetu,” alisema Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Mkuu aliwataka wananchi kuheshimu mipango ya matumizi ya ardhi kwa kuepuka kujenga nyumba za kudumu ndani ya eneo hilo, akisisitiza kuwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha migogoro isiyo ya lazima.
“Tunawaomba wananchi msijenge nyumba za kudumu katika eneo hili. Tuendelee kushirikiana na jeshi ili matumizi ya eneo hili yaweze kuwanufaisha wananchi na wakati huo huo kusaidia shughuli za mafunzo ya majeshi yetu,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama ni muhimu katika kulinda rasilimali za taifa na kudumisha amani na utulivu nchini.
Mkutano huo wa hadhara ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na chama pamoja na mamia ya wananchi wa Monduli waliopata fursa ya kusikiliza maelezo ya viongozi wao na kuwasilisha changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.
Ends


0 Comments