RUTO ATAKA EAC IHARAKISHE USHIRIKIANO, IIMARISHE UCHUMI WA KIKANDA, YABANA MATUMIZI WABUNGE EALA KULIPWA MISHAHARA NA NCHI ZAO
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Rais wa Kenya, William Ruto, ametoa wito kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuongeza mshikamano na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya pamoja ya maendeleo ili kuifanya Afrika Mashariki kuwa moja ya kanda zenye uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika.
Ruto alitoa kauli hiyo wakati akifungua Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika jijini Arusha, akisisitiza kuwa mustakabali wa wananchi wa ukanda huo unategemea uwezo wa viongozi wa nchi wanachama kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Alisema EAC imeendelea kuwa mfano wa mafanikio ya ushirikiano wa kikanda barani Afrika, lakini bado kuna haja ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa makubaliano na sera mbalimbali zilizopitishwa ili wananchi waweze kunufaika moja kwa moja na matunda ya jumuiya hiyo.
“Ushirikiano wetu si chaguo bali ni hitaji muhimu kwa maendeleo ya watu wetu. Tunapaswa kuongeza juhudi katika kukuza biashara, uwekezaji, miundombinu na fursa za ajira kwa vijana wetu,” alisema Ruto.
Katika hotuba yake, Ruto alisisitiza kuwa kukuza biashara ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki ni moja ya vipaumbele vikubwa vya jumuiya hiyo, akieleza kuwa ushirikiano wa kiuchumi utaongeza uwezo wa nchi wanachama kushindana katika soko la kimataifa.
Alibainisha kuwa juhudi za kuondoa vikwazo visivyo vya ushuru, kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuunganisha mifumo ya biashara kati ya nchi wanachama zitasaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa kikanda.
Kwa mujibu wa Ruto, kuimarishwa kwa muungano wa forodha pamoja na soko la pamoja la Afrika Mashariki kutachochea uwekezaji mkubwa zaidi katika sekta mbalimbali za uchumi, huku biashara ya ndani ya ukanda huo ikitarajiwa kuongezeka kwa kiwango kikubwa katika miaka ijayo.
Akizungumzia sekta ya miundombinu, Ruto alisema jumuiya hiyo imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kurahisisha usafirishaji wa watu na mizigo katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Alitaja miradi ya reli ya kisasa ya umeme nchini Tanzania kuwa moja ya mifano ya mafanikio ya uwekezaji wa miundombinu ndani ya ukanda huo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, reli hiyo ya kisasa iliyoanza kufanya kazi Juni 14, 2024, imekuwa ikisafirisha wastani wa abiria zaidi ya 10,000 kwa siku kati ya Dar es Salaam na Dodoma, huku huduma ya usafirishaji mizigo ikianza rasmi Juni 27 mwaka jana kutoka Bandari ya Dar es Salaam kupitia kituo cha reli cha Bubu hadi Ihumwa.
Alisema hatua hiyo imeongeza ufanisi katika usafirishaji wa bidhaa na kurahisisha biashara ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Aidha, Ruto alieleza kuwa juhudi za kuimarisha usafiri wa majini katika Ziwa Victoria zimeanza kuzaa matunda baada ya meli mpya za mizigo kuanza kufanya kazi katika ukanda huo, hali iliyoongeza uwezo wa kusafirisha mizigo hadi kufikia tani 890,000 kwa mwaka.
Katika sekta ya utalii, Ruto alisema nchi wanachama wa EAC zinaendelea kutangaza ukanda huo kama kituo kimoja cha utalii duniani, hatua inayolenga kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Afrika Mashariki.
Alisema jumuiya hiyo pia imeanza kuimarisha uchumi wa michezo baada ya nchi za Kenya, Uganda na Tanzania kuungana katika maandalizi ya mashindano makubwa ya soka ya Afrika.
Kwa mujibu wa Ruto, ukanda huo unaendelea kuwekeza katika miundombinu ya michezo kwa lengo la kujiandaa kuandaa mashindano ya Africa Cup of Nations 2027, ambayo yanatarajiwa kufungua fursa nyingi za ajira kupitia sekta ya michezo.
Katika eneo la teknolojia, alisema jumuiya hiyo imeanza hatua muhimu kuelekea kuanzisha soko moja la kidijitali, hatua itakayosaidia kukuza uchumi wa kidijitali na kuongeza ushindani wa ukanda huo katika uchumi wa dunia.
Pamoja na mafanikio hayo, Ruto alikiri kuwa bado kuna changamoto kadhaa zinazoikabili kanda hiyo, hususan katika masuala ya usalama.
Alitaja hali ya migogoro katika maeneo ya mashariki mwa Democratic Republic of the Congo kuwa inahitaji ushirikiano wa pamoja wa kikanda na kimataifa ili kufikia suluhu ya kudumu.
Alisisitiza kuwa maendeleo ya kiuchumi hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa amani na utulivu wa kisiasa katika ukanda huo.
“EAC itaendelea kushirikiana na taasisi za kikanda na kimataifa kuhakikisha amani na utulivu vinarejeshwa katika maeneo yenye migogoro,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, wakuu wa nchi wanachama wa EAC wamekubaliana kubadili mfumo wa michango ya kifedha ya nchi wanachama ili kuimarisha uwezo wa kifedha wa jumuiya hiyo.
Chini ya mfumo mpya, asilimia 50 ya mchango wa kila nchi itakuwa sawa kwa wanachama wote, huku asilimia 50 ikitegemea ukubwa wa uchumi wa kila nchi.
Aidha, viongozi hao wameamua pia kupunguza gharama za uendeshaji wa jumuiya hiyo kwa kubadili mfumo wa ulipaji wa mishahara ya wabunge wa East African Legislative Assembly (EALA).
Kwa utaratibu mpya, mishahara ya wabunge hao italipwa na mabunge ya nchi walizochaguliwa badala ya kulipwa na EAC moja kwa moja, hatua inayotarajiwa kupunguza karibu asilimia 30 ya matumizi ya bajeti ya jumuiya hiyo.
EAC itaendelea kulipia posho za wabunge hao wanaposhiriki shughuli rasmi za jumuiya hiyo.
Akihitimisha hotuba yake, Ruto alisema juhudi za kufikia malengo ya muda mrefu ya EAC zinapaswa kuendelea kwa kasi, ikiwemo kuimarisha soko la pamoja, muungano wa forodha na hatimaye kufikia ndoto ya shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki.
Alisema wananchi wa kanda hiyo wanatarajia kuona matokeo ya haraka ya ushirikiano huo, hususan katika sekta za biashara, miundombinu, teknolojia na ajira.
“Kwa mshikamano wetu, tunaweza kujenga Afrika Mashariki yenye uchumi imara, amani ya kudumu na fursa pana kwa kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Ruto.
Ends..












0 Comments