MEYA ARUSHA ACHACHAMAA,AONYA WAKANDARASI UCHELEWESHAJI WA MIRADI MIKUBWA YA MABILIONI ,ADAI HAKUTAKUWA NA NYONGEZA YA MUDA HADI MEI-2026 IWE IMEKAMILIKA

 Na Joseph Ngilisho – Arusha


UONGOZI wa Halmashauri ya Jiji la Arusha umeweka msimamo mkali kwa wakandarasi na wasimamizi wa miradi ya maendeleo, ukisisitiza kuwa hakuna nyongeza ya muda itakayoruhusiwa kwa miradi yote ya kimkakati inayotekelezwa jijini humo, hatua inayolenga kulinda thamani ya fedha za umma na kuhakikisha wananchi wananufaika kwa wakati.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mstahiki Meya wa Jiji hilo, Maximilian Iranghe, amesema msimamo huo umetokana na maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, aliyefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo jijini humo na kuagiza ikamilike kwa mujibu wa ratiba bila visingizio.


Iranghe amesema katika ziara hiyo ya kimkakati, Prof. Shemdoe alikagua miradi kadhaa ikiwemo Stendi ya Bondeni iliyopo Kata ya Olasiti, Uwanja wa Michezo wa Jiji la Arusha pamoja na Soko la Kilombero, ambako alijionea hatua mbalimbali za utekelezaji.


Kwa mujibu wa Meya huyo, Stendi ya Bondeni na Soko la Kilombero zimefikia asilimia 40 ya utekelezaji, hali iliyomfanya waziri kupongeza juhudi zinazofanywa, huku akiwataka wasimamizi na wakandarasi kuongeza kasi ili kufikia malengo yaliyowekwa. Aidha, alieleza kuwa kasi ya ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Jiji la Arusha imeridhisha na kupongezwa rasmi na waziri.


Iranghe amesisitiza kuwa miradi ya Stendi ya Bondeni, Soko la Kilombero, Soko la Kwa Mrombo pamoja na eneo la mapumziko imepangwa kukamilika ifikapo Mei 26, 2026, na kwamba tarehe hiyo ni ya mwisho bila uwezekano wa kuongeza muda.


“Tumepokea maelekezo ya waziri na kama jiji tumesimama imara. Hakutakuwa na nyongeza ya muda; tutashirikiana na wakandarasi na wasimamizi kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati uliopangwa,” alisema Iranghe.


Ameeleza kuwa, licha ya changamoto ndogondogo zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa miradi, hakuna uhalali wa kuchelewa kwa kuwa miradi hiyo ni ya mwaka mmoja na tayari imepiga hatua kubwa, hususan katika kazi za msingi ambazo kwa kawaida huchukua muda mrefu.


“Kilichobaki kwa kiasi kikubwa ni kazi za juu ambazo ni rahisi kutekelezwa kwa muda mfupi. Hakuna danadana, miradi ipo kwenye ratiba na lazima ikamilike kwa wakati,” alisisitiza.


Meya Iranghe amehitimisha kwa kutoa wito kwa wakandarasi, wasimamizi wa miradi na watendaji wote kuongeza bidii, nidhamu na uwajibikaji ili miradi hiyo ikamilike kwa viwango vinavyokubalika na kuleta tija kwa wananchi wa Jiji la Arusha.


Ends..

Post a Comment

0 Comments