RC MAKALA ATAKA USHIRIKIANO NA WADAU KUFANIKISHA BIMA YA AFYA KWA PAMOJA

 Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

RC Makalla: Ushirikiano wa Wadau Ni Msingi Utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote


Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, amesema utekelezaji wenye tija wa Bima ya Afya kwa Wote unahitaji ushiriki wa wadau kutoka sekta zote ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanajiunga na mifuko ya bima ya afya, kama alivyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Akizungumza leo Alhamisi, Desemba 18, 2025, wakati wa kikao cha uelimishaji na uhamasishaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kilichofanyika mkoani Arusha, CPA Makalla alisisitiza kuwa kujiunga na bima ya afya ni nguzo muhimu ya kumwezesha kila Mtanzania kupata huduma bora za matibabu kwa wakati, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.


“Hadi sasa Mkoa wa Arusha una jumla ya wakazi wapatao 2,356,255, lakini waliokwisha jiunga na mifuko ya bima ya afya ni 353,438 tu, sawa na asilimia 15. Takwimu hizi zinaonesha wazi kuwa bado kuna kazi kubwa ya kuhamasisha jamii,” amesema CPA Makalla. Ameongeza, “Nawasihi mshiriki kikamilifu kikao hiki ili mpate uelewa wa kutosha na kwenda kuwa mabalozi wa kuelimisha wananchi wengine.”


Akiendelea kufafanua faida za Bima ya Afya kwa Wote, Mkuu huyo wa Mkoa amesema mchangiaji atapata huduma za matibabu katika kituo chochote nchini, huku vituo vya afya vikinufaika kwa kuwa na uhakika wa mapato yatakayowezesha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi pamoja na uwepo wa wataalamu wa kutosha na wenye ujuzi.


Katika kikao hicho, mada mbalimbali ziliwasilishwa kwa lengo la kuongeza uelewa kwa washiriki kuhusu dhana ya Bima ya Afya kwa Wote, maudhui ya Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, maeneo yaliyotiliwa mkazo katika sheria hiyo, pamoja na uboreshaji wa mifumo ya ukusanyaji wa fedha na taarifa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.


Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unafikiwa kwa ufanisi na wananchi wengi zaidi wanapata huduma bora za afya kwa gharama nafuu na kwa uhakika


.

Post a Comment

0 Comments