👉 UTEUZI
Na Mwandishi Wetu- Arushadigital
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, ameteuliwa na Baraza Kuu la Wazazi Taifa kuwa Mjumbe wa Kamati Ndogo ya Mipango, Uchumi, Uwekezaji na Fedha, uteuzi unaoonesha imani kubwa ya jumuiya hiyo katika uwezo wake wa kiuongozi na kitaaluma.
Kwa mujibu wa taarifa ya uteuzi huo, Baraza Kuu la Wazazi Taifa limezingatia vigezo mbalimbali muhimu kabla ya kumchagua Dkt. Lukumay, vikiwemo uanachama wake hai ndani ya Chama na Jumuiya, sifa za kielimu, pamoja na uelewa mpana wa malengo makuu na dira ya Jumuiya ya Wazazi Taifa.
Vigezo vingine vilivyozingatiwa ni pamoja na utayari wake wa kujitolea kutekeleza majukumu ya kamati bila kutegemea malipo, mchango wa hali na mali katika kufanikisha shughuli na malengo ya Jumuiya, pamoja na uadilifu, maadili mema na rekodi ya uwajibikaji katika nafasi mbalimbali alizowahi kuzihudumia.
Aidha, Baraza hilo limeeleza kuwa mtandao mpana wa Dkt. Lukumay kikazi na kimaisha ni rasilimali muhimu inayoweza kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi na uwekezaji, na hivyo kusaidia Jumuiya ya Wazazi Taifa kusimamia na kutekeleza kwa ufanisi malengo yake ya msingi.
Uteuzi huo unatarajiwa kuimarisha zaidi mipango ya kiuchumi, uwekezaji na usimamizi wa fedha ndani ya Jumuiya ya Wazazi Taifa, sambamba na mchango wa maendeleo ya elimu na ustawi wa jamii kwa ujumla.

0 Comments