KAMPUNI YA RADDY ENERGY YA TANZANIA KUNUNUA MITAMBO YA UZALISHAJI UMEME KUTOKA KAMPUNI YA SIEMENS YA USWIDI KWA DOLA MILIONI 320

KAMPUNI YA RADDY ENERGY YA TANZANIA KUNUNUA MITAMBO YA UZALISHAJI UMEME KUTOKA KAMPUNI YA SIEMENS YA USWIDI KWA DOLA MILIONI 320

Na Arushadigital – Stockholm

Kampuni ya Raddy Energy Solution Limited ya Tanzania imeingia makubaliano makubwa ya kimkakati na kampuni ya Siemens Energy ya Uswidi kwa ununuzi wa mitambo minne ya kisasa ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia, yenye jumla ya uwezo wa megawati 177, kwa gharama ya dola za Marekani milioni 320.


Hatua hiyo inaashiria uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati nchini na inaelezwa kuwa ni sehemu ya mpango mpana wa Raddy Energy wa kuongeza uzalishaji wa umeme wa uhakika, safi na endelevu kwa matumizi ya ndani na masoko ya kikanda.


Kwa mujibu wa makubaliano hayo, mitambo hiyo inatarajiwa kuwasili nchini Tanzania na kufungwa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2027. Ununuzi huo umewezeshwa na Benki ya CRDB kama mshirika wa ndani katika upangaji na uratibu wa kifedha wa mradi. Raddy Energy ni kampuni dada na kiwanda cha Raddy Fibers kilichopo Mkuranga, mkoani Pwani.


Katika utekelezaji wa mradi huo, Benki ya CRDB itashirikiana kwa karibu na taasisi mbalimbali za fedha za Serikali ya Uswidi, zikiwemo Wakala wa Mikopo ya Mauzo ya Nje wa Uswidi (EKN), Shirika la Mikopo ya Mauzo ya Nje la Uswidi (SEK), Taasisi ya Fedha za Maendeleo ya Uswidi (Swedfund), Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Uswidi (SIDA) pamoja na Taasisi ya Mauzo ya Nje na Uwekezaji ya Uswidi (Business Sweden).


Aidha, Baraza la Kimataifa la Viwanda la Uswidi (NIR) litatoa ushauri wa kitaalamu kwa timu ya kimataifa itakayohakikisha mradi huo unatekelezwa kwa viwango vya juu vya ubora. Mradi huo unatajwa kuwa ni hatua ya mwanzo tu, kwani Raddy Energy imeweka mkakati wa kufikisha uwezo wa uzalishaji wa umeme hadi megawati 1,000 ifikapo mwaka 2030, lengo likiwa ni kuimarisha usalama wa nishati nchini na kuiwezesha Tanzania kuuza umeme nje ya nchi.


Katika kuimarisha ushirikiano huo, watendaji wa Raddy Energy walifanya ziara ya kimkakati nchini Uswidi kuanzia tarehe 10 hadi 13 Desemba, 2025, chini ya uratibu wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo. Ziara hiyo ilijumuisha mikutano na viongozi wa Siemens Energy pamoja na taasisi za fedha za Serikali ya Uswidi, iliyofanyika katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje jijini Stockholm, na baadaye ujumbe huo kuzuru makao makuu ya Siemens mjini Finspäng.


Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uswidi, Mhe. Mobhare Matinyi. Kampuni ya Raddy Energy iliwakilishwa na Mwanzilishi na Mkurugenzi Mwendeshaji, Bw. Ramadhan Hassan Mlanzi, pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara na Miradi, Bw. Ediphine Masase. Kwa upande wa Benki ya CRDB, timu ya miradi mikubwa iliongozwa na Bw. Musa Lwila, Bw. Saidi Salehe na Bw. Andrew Mbunda.


Kwa upande wa Siemens Energy, kikao hicho kilihusisha Mkurugenzi wa Ufadhili wa Miradi, Bw. Joakim Tornberg na Meneja Mwandamizi wa Mauzo, Bi. Christiane Carlsson. Timu ya Serikali ya Uswidi iliongozwa na Mshauri Mwandamizi wa Biashara na Uendelezaji kwa Bara la Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Bi. Pia Roed.


Wawakilishi wengine wa taasisi za Serikali ya Uswidi walijumuisha Bi. Anna Liberg (Business Sweden), Bw. Maximilian Jönsson (SIDA), Bw. Johan Heiskala (Swedfund), Bw. Klas Lindgren (EKN), Bw. Pontus Davidsson (SEK) na Bi. Christine Bäckström (NIR).


Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Matinyi alisisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania katika kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi na Uswidi, akibainisha kuwa Tanzania ina fursa kubwa za uwekezaji katika sekta za madini, viwanda, kilimo cha biashara, usafirishaji, utalii pamoja na teknolojia na ubunifu.

Pichani -Kikao cha pamoja baina ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uswidi, kampuni ya Raddy Energy, Benki ya CRDB na wawakilishi wa taasisi za fedha za Serikali ya Uswidi wakiendelea na kikao jijini Stockholm, hivi karibuni.

Imetolewa na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uswidi

Stockholm, Desemba 19, 2025

Ends...

Post a Comment

0 Comments