MBUMBE DKT LUKUMAY ACHAFUKWA AAGIZA KILA DIWANI KUMPA ORODHA YA VITONGOJI VISIVYO NA NISHATI YA UMEME KWENYE KATA ZAO,ATAKA AKABIDHIWE KABLA YA BUNGE LA JANUARI

 SERIKALI YAPELEKA UMEME KILA KIJIJI ARUMERU MAGHARIBI, VITONGOJI 58 BADO – LUKUMAY

Na Joseph Ngilisho-ARUMERU

MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika sekta ya umeme hatua iliyowezesha vijiji vyote 67 vya jimbo hilo kufikiwa na nishati ya umeme, huku jitihada zikiendelea kuhakikisha vitongoji vilivyosalia vinaunganishwa haraka iwezekanavyo.


Akizungumza leo desemba 19,2025 na wananchi na viongozi wa ngazi mbalimbali katika kata ya Mlangarini, Dkt. Lukumay alisema kati ya vitongoji 259 vilivyopo jimboni humo, vitongoji 201 tayari vina umeme, huku vitongoji 58 vikiwa bado havijaunganishwa. Alisisitiza kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha hakuna kitongoji kinachosalia bila huduma hiyo muhimu.


“Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye umeme. Vijiji vyote 67 vina umeme, na sasa tunashughulikia vitongoji vilivyosalia ili navyo vipate huduma hii,” alisema Dkt. Lukumay.


Katika hatua nyingine, aliwataka madiwani wote wa kata za jimbo hilo kuwasilisha kwa haraka taarifa sahihi za idadi ya vitongoji ambavyo bado havina umeme pamoja na mahitaji ya nguzo za umeme, ili taarifa hizo ziwasilishwe kabla ya Bunge lijalo linalotarajiwa kuketi mapema Januari 2026.


“Nawaomba madiwani wote wa jimbo langu waanze kuandika idadi ya vitongoji visivyo na umeme na idadi ya nguzo za umeme zinazohitajika kabla ya Bunge lijalo la Januari,” alisisitiza.


Aidha, Dkt. Lukumay aliwataka madiwani na viongozi wa maeneo husika kuhamasisha wananchi kuanza maandalizi ya ndani ya nyumba zao kwa kutengeneza miundombinu ya waya za umeme, ili pindi umeme utakapofika, waweze kuunganishwa mara moja na huduma hiyo iingie moja kwa moja majumbani.


Kuhusu changamoto za miundombinu, Mbunge huyo alisema barabara bado ni kikwazo kikubwa katika jimbo la Arumeru Magharibi, akieleza kuwa tayari amewasilisha hoja hiyo kwa Waziri mwenye dhamana ya ujenzi alipokutana naye, ili hatua za haraka zichukuliwe.


Pia alibainisha kuwepo kwa changamoto ya vivuko, akisema jumla ya vivuko 136 vinahitajika ili kuwawezesha wananchi kuvuka maeneo hatarishi kwa usalama katika misimu yote ya mwaka.


Kwa upande wa huduma za kijamii, Dkt. Lukumay alisema changamoto zinazohusu maji, elimu na afya—ikiwemo shule na hospitali—zinaendelea kufanyiwa kazi kwa umakini mkubwa, kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha wananchi wa Arumeru Magharibi wanapata huduma bora na za uhakika.


Alisisitiza kuwa ataendelea kusimamia na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo ili kuhakikisha inaleta tija na kuboresha maisha ya wananchi wa jimbo hilo.

Ends..

Post a Comment

0 Comments