MAHAFALI YA 27 CHUO CHA UHASIBU ARUSHA IAA,SERIKALI YAPONGEZA KITUO KINARA CHA ELIMU YA FEDHA NCHINI,WAHITIMU 4821 WATUNUKIWA

Mahafali ya 27 IAA: Serikali Yapongeza Kituo Kinara cha Elimu ya Fedha

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA


CHUO cha Uhasibu Arusha (IAA) kimeendelea kuthibitisha nafasi yake kama kimbilio la elimu ya juu yenye ubora, maadili na weledi, huku serikali ikiipongeza kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya taifa. 


Hayo yalisemwa leo desemba 19,2025 na Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde , wakati wa Mahafali ya 27  yaliyofanyika  chuoni hapo ambapo jumla ya wahitimu wapatao 4821 wametunukiwa vyeti.

Akizungumza mbele ya viongozi wa serikali, viongozi wa dini, wazazi, wahadhiri na wahitimu, Mhandisi Munde alisema IAA imejipanga kuhakikisha wahitimu wake wanakuwa job-ready, wakiwa na ujuzi wa kisasa unaokidhi mahitaji ya soko la ajira katika sekta za fedha, uhasibu, TEHAMA, benki, bima, masoko na usimamizi wa biashara.


"Serikali inatambua mchango wa IAA katika kutoa mafunzo, ushauri wa kitaalam na utafiti unaochangia katika sera na maendeleo ya jamii. Huu ni mfano wa chuo kinachoelekeza maarifa yake moja kwa moja kwenye huduma kwa taifa," alisema Munde.


Naibu Waziri pia aliwapongeza viongozi wa IAA kwa kuboresha mitaala, kuanzisha smart classrooms, maabara za TEHAMA, na miundombinu ya kisasa katika kampasi za Arusha, Babati na Songea, hatua iliyoongeza uwezo wa chuo kupokea idadi kubwa ya wanafunzi na kutoa elimu ya kiwango cha kimataifa.


Mhandisi Munde alisisitiza umuhimu wa wahitimu kuwa wabunifu, waadilifu na wenye mchango katika jamii, akiwashauri kutumia maarifa waliyopata kuchochea maendeleo ya familia zao na taifa kwa ujumla.


Mahafali hayo pia yalihudhuriwa na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo, Dkt. Mwamini Tulli, ambaye aliwapongeza wahitimu na kuhimiza utumishi wa kitaaluma unaochangia maendeleo ya Taifa.

Dkt. Tulli alibainisha kwamba mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za pamoja za serikali, menejimenti ya chuo, wahadhiri, wazazi na wanafunzi.


Jumla ya wahitimu 4,821 walitunukiwa vyeti mbalimbali, ikiwa ni ongezeko la wahitimu 308 ikilinganishwa na mwaka jana. Kati yao, wanaume walikuwa 2,810 na wanawake 2,011, huku wahitimu wa Shahada wakihesabiwa 1,572, Stashahada ya Juu 3, Stashahada 1,035 na Astashahada 1,713.


Awali Prof. Eliamani Sedoyeka, Mkuu wa Chuo, alisema mafanikio haya hayangewezekana bila ushirikiano wa Baraza la Uongozi, wafanyakazi, wahadhiri, wazazi na wadhamini. 


Alibainisha jitihada za chuo za kuanzisha mitaala mipya yenye lengo la kukuza ujuzi wa vitendo na ubunifu, ikiwemo Usimamizi wa Mnyororo wa Thamani katika Kilimo, Usalama wa Mtandao (Cyber Security), na Fedha na Uwekezaji.



Aidha, Prof. Sedoyeka alifafanua hatua za chuo katika kutumia TEHAMA kwa madarasa janja (Smart Classes) na kampasi janja (Smart Campus), pamoja na kushirikiana na vyuo vikuu vya kimataifa kama Chuo Kikuu cha Heriot Watt, Uingereza, ili kuboresha mitaala na utafiti.



Sherehe za mahafali hayo ziliashiria mafanikio makubwa ya chuo katika kutoa elimu bora, utafiti wa kitaalamu, na kuandaa vijana kuwa watumishi wa umma na wa biashara wenye uwezo na ujuzi wa kimataifa.


Wahitimu hao ambao walitunukiwa vyeti na mgeni rasmi ,wametakiwa kuwa mabalozi bora wa IAA, wakihimizwa kutumia elimu waliyoipata kwa uadilifu, bidii, ubunifu na uwajibikaji.







Ends..

Post a Comment

0 Comments