PINDA AAGIZA KUBORESHA KWA MFUMO MPYA WA KURATIBU TAFITI ZA KILIMO

Pinda Aagiza Kuanzishwa Mfumo Mpya wa Kuratibu Tafiti za Kilimo

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA


WAZIRI Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, ameagiza kuanzishwa kwa mfumo maalum wa ukusanyaji na uratibu wa tafiti za kilimo ili kuiwezesha serikali kuzichambua kwa ufanisi, kubaini athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao nchini.

Akizungumza  leo dec 4,2025 jijini Arusha wakati akifungua Mkutano wa Nne wa Mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Sayansi za Mazao (CROSAT), Pinda alisema mfumo huo utakapowekwa na kusimamiwa kikamilifu, utaisaidia serikali kuwa na taarifa sahihi za tafiti kutoka kila mkoa na hivyo kupanga mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili wakulima.

Alisema serikali imeendelea kuimarisha sekta ya utafiti nchini, ikiwemo kuitengea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kiasi cha shilingi bilioni 40.73, fedha ambazo zimewezesha kuzalishwa kwa teknolojia mpya 64 zinazolenga kuongeza ufanisi, tija na ustahimilivu wa mazao dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

> “Endapo tafiti zote zitaingizwa kwenye mfumo maalum, serikali itabaini kwa urahisi changamoto za wakulima katika kila eneo na kuchukua hatua stahiki. Hii itasaidia kukuza ajira na kuongeza mchango wa kilimo katika uchumi wa taifa,” alisema Pinda.


Aidha, Pinda alibainisha kuwa juhudi zinazofanywa na serikali katika kukuza sekta ya kilimo zimeiwezesha Tanzania kufikia asilimia 128 ya uzalishaji wa chakula, kiwango kinachozidi mahitaji ya ndani na kuruhusu ziada kuuzwa nje ya nchi.

Waziri Mkuu huyo Mstaafu pia alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuimarisha menejimenti ya programu ya Building a Better Tomorrow (BBT) ili iwafikie vijana wengi zaidi, hususan wa vijijini, hatua itakayochochea mageuzi ya kilimo kuelekea malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Kwa upande wake, Rais na Mwenyekiti wa CROSAT, Profesa Kalunde Sibuga, alisema chama hicho kwa sasa kina wanachama 294 kutoka sekta binafsi, taasisi za utafiti, mashirika na wataalamu mbalimbali wa sayansi za mazao.

Profesa Sibuga alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya wataalamu na serikali ili kuimarisha sekta ya kilimo, kuongeza ajira na kuhakikisha matumizi ya teknolojia za kisasa yanachochea ustahimilivu wa mazao dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.





Ends

Post a Comment

0 Comments