EU YASIKITISHWA NA MAUAJI TANZANIA YATAKA MIILI IKABIDHIWE KWA NDUGU

EU, Uingereza na Canada waikumbusha Tanzania kutekeleza ahadi za kulinda haki za msingi

By Arushadigital


Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) nchini Tanzania kwa ushirikiano na Serikali za Uingereza na Canada, umetaka Serikali ya Tanzania kutekeleza kikamilifu ahadi zake za kimataifa kuhusu kulinda haki za msingi za wananchi, ikiwemo haki ya kupata taarifa na uhuru wa kujieleza kama ilivyoainishwa katika Katiba ya nchi.


Wito huo umetolewa leo Desemba 5, 2025 kupitia tamko la pamoja la EU, likirejea kauli ya Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya pamoja na tamko la pamoja la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Norway na Uingereza lililotolewa Oktoba 31, 2025 kuhusu Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29.


Kwa mujibu wa tamko hilo, EU imeeleza kusikitishwa na taarifa za vifo na idadi kubwa ya majeruhi waliotokana na matukio ya vurugu wakati wa Uchaguzi Mkuu. 


Umoja huo umebainisha kuwa taarifa kutoka mashirika ya kitaifa na kimataifa zinatoa ushahidi wa matukio ya mauaji kinyume cha utaratibu wa kisheria, kupotea kwa watu, ukamataji holela pamoja na madai ya kufichwa kwa miili ya waliofariki.


EU na washirika wake wametoa wito kwa mamlaka husika kukabidhi miili ya marehemu kwa familia zao, kuwaachia huru wote wanaotajwa kuwa wafungwa wa kisiasa, na kuhakikisha waliokamatwa wanapata msaada wa kisheria na huduma za matibabu.


Aidha, Umoja huo umeitaka Serikali ya Tanzania kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti za awali za waangalizi wa Uchaguzi kutoka Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambazo zilibainisha mapungufu mbalimbali yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi.


“Tunaipongeza hatua ya Serikali kukiri kuwa uelewa wa kiini na mazingira yaliyopelekea vurugu na vifo ni msingi muhimu kuelekea upatikanaji wa haki na maridhiano. Hata hivyo, uchunguzi wowote lazima uwe huru, wazi na shirikishi, ukijumuisha asasi za kiraia, taasisi za kidini na wadau wote wa kisiasa,” tamko hilo limeeleza.


#ArushaDigital

Post a Comment

0 Comments