IRANGHE AREJEA KWA KISHINDO U-MEYA ARUSHA,DC MKUDE ATAKA MADIWANI WAZINGATIE UADILIFU NA UWAJIBIKAJI,TIZAMA PICHA WALIVYOAPA

Na Joseph Ngilisho – Arusha

BARAZA jipya la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha limezinduliwa rasmi leo mbele ya mamia ya wananchi, likishuhudia jumla ya madiwani 34—wakiwemo 25 wa kuchaguliwa na tisa wa viti maalum—wakila kiapo cha utii, uadilifu na uwajibikaji, tayari kuanza safari ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Hafla hiyo iliyoongozwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Boniface Semroki ilitawaliwa na shangwe, hamasa na matumaini mapya kutoka kwa wananchi waliokusanyika kushudia viongozi wao wakianza rasmi majukumu ya utumishi wa umma.


Akizungumza mara baada ya madiwani kuapishwa, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, aliwataka viongozi hao wapya kuheshimu na kutekeleza kwa vitendo kiapo walichokula, akisisitiza kuwa msingi wa maendeleo ni uadilifu, sheria na amani.

> “Mmeapa kuwatumikia wananchi. Hakikisheni mnatekeleza yale mliyowaahidi. Ondoeni chuki, dalilieni amani na mshikamano kwa kuwa maendeleo hayapatikani bila utulivu,” alisema Mkude.


DC Mkude aliwakumbusha kuwa nafasi waliyopewa ni heshima kubwa na dhamana ya wananchi kuwatumainia katika kusimamia huduma muhimu na miradi ya maendeleo.


Katika uchaguzi uliofanyika ndani ya baraza hilo, aliyekuwa Meya wa Jiji la Arusha Maxmillian Iranqhe aliibuka tena na ushindi mkubwa kwa kupata kura 33 kati ya 34, huku Julius Meideye akichaguliwa kuwa Naibu Meya kwa kura 31 kati ya 34.

Akitoa hotuba yake ya uzinduzi wa baraza, Meya Iranqhe aliwashukuru madiwani kwa imani yao na kuahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa ilani ya CCM na mipango ya maendeleo ya jiji.

> “Tutaanzia pale tulipoishia. Kipaumbele chetu ni matengenezo ya barabara, usafi wa jiji na kuboresha mazingira. Tunataka Arusha iwe jiji la mfano nchini,” alisema Iranqhe.


Aidha alisisitiza umuhimu wa kuwekeza kwa vijana, akisema idadi ya wakazi wa jiji hilo inakadiriwa kufikia zaidi ya 600,000, ambapo vijana ni asilimia 60 ya wakazi wote.

> “Tuweke mazingira rafiki ya fursa za kiuchumi kwa vijana. Hawa ndiyo nguvu kazi ya jiji letu, na tukiwapa nafasi sahihi wataliinua Arusha kimaendeleo,” aliongeza.

Awali, Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Jacob Rombo, aliwapongeza madiwani walioteuliwa na kuchaguliwa, akiwataka wajikite kwenye utendaji wenye tija kwa jamii.

Alisema wakati madiwani walipokuwa nje, Mkurugenzi wa Jiji, John Kayombo, pamoja na wakuu wa idara walihakikisha shughuli za huduma kwa wananchi zinaendelea bila kuathirika.

> “Mnarejea kwenye majukumu yenu wakati ambao jiji limeendelea kufanya kazi kwa ufanisi. Endeleeni kushirikiana na watumishi wetu kwa misingi ya sheria na taratibu,” alisema Rombo.

Katika ujumla wa hotuba za viongozi, kauli kuu iliyojitokeza ni wito wa mshikamano, kuepuka migogoro, kuheshimu sheria na kuweka mbele maslahi ya wananchi kuliko siasa.

Wananchi waliokuwepo kwenye mkutano huo walionesha matumaini mapya kwa baraza hilo jipya, wakitarajia maboresho ya huduma, usimamizi madhubuti wa miradi, na kasi mpya ya maendeleo katika Jiji la Arusha.



















Post a Comment

0 Comments