DIWANI KISONGO AAHIDI KUSUKUMA MAENDELEO KWA NGUVU ZOTE,AANZA KWA KASI YA 5G KWA KUPANGA VIPAUMBELE VIKUU


DIWANI KISONGO AAHIDI KUSUKUMA MAENDELEO KWA NGUVU ZOTE, AANZA KWA KASI YA 5G KUPANGA VIPAUMBELE VIKUU

Na Joseph Ngilisho – Arumeru

DIWANI wa Kata ya Kisongo, Violet Ngowo, ameahidi kusimamia kwa nguvu zote utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata hiyo, ikiwemo miundombinu ya barabara, upatikanaji wa maji, huduma za afya, elimu na mikopo ya uwezeshaji kwa vijana na wanawake.

Akizungumza mara baada ya kuapishwa katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Arusha lililoanza rasmi leo Desemba 2, 2025, diwani huyo alisema kuwa kuanza kwa baraza hilo ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa ahadi walizotoa wakati wa kampeni.

> “Tunamshukuru Mungu. Leo tarehe 2 Desemba 2025 baraza letu limeanza rasmi katika Jimbo la Arumeru Magharibi, Halmashauri ya Arusha. Kama madiwani tumeweka vipaumbele vingi vya maendeleo, na kama diwani wa Kisongo nitahakikisha barabara, maji, afya, shule na maisha ya wananchi, ikiwemo mikopo kwa vijana na wanawake, vinapewa kipaumbele,” alisema Ngowo.



Aidha, alieleza kuwa baada ya baraza hilo kuapishwa rasmi na kupata Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, madiwani sasa wako tayari kuanza kazi kwa kufuata Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya 2025/2035.

> “Wananchi wategemee utekelezaji wa kile tulichowaahidi. Ahadi hazikuwa za kampeni tu, bali ni sehemu ya ilani inayotakiwa kutekelezwa,” aliongeza.


Ngowo pia alibainisha kuwa Kata ya Kisongo bado inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohitaji suluhisho la haraka, na akaeleza dhamira yake ya kushirikiana na madiwani wengine pamoja na Halmashauri kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo wanayostahili.

-ends..

Post a Comment

0 Comments