MAKALLA AWASHA MOTO KASI YA UJENZI WA BARABARA YA MIANZINI–NGARAMTONI
Na Joseph Ngilisho, Arumeru
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, ameendelea kuifuatilia kwa karibu miradi ya miundombinu mkoani humo baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Mianzini – Timbolo – Olemringaringa – Ngaramtoni – Selian yenye urefu wa kilomita 18.
Barabara hiyo inayotekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 23 ni miongoni mwa miradi mikubwa ya Serikali inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma, kukuza uchumi wa maeneo ya pembezoni na kurahisisha muunganiko wa kata mbalimbali na jiji.
Katika ukaguzi wake, Makalla alimtaka mkandarasi STECOL Corporation kuongeza msukumo wa kazi ili kukamilisha mradi kwa wakati, akisisitiza kuwa Serikali imeshatimiza wajibu wake kwa kutoa fedha zote za utekelezaji.
“Serikali imetekeleza wajibu wake kikamilifu, sasa kazi iko kwa mkandarasi. Wananchi wanahitaji kuona matokeo, na barabara hii ni kiungo muhimu kwa shughuli zao za kila siku,” alisema Makalla.
Amesema changamoto ya fidia sasa imeondoka baada ya wananchi kulipwa Sh bilioni 3.5, hivyo hakuna sababu ya mradi kuendelea kusuasua.
Kwa upande wake, msimamizi wa mradi kutoka STECOL, Yuan Rui, alisema kampuni yake imeimarisha nguvu kazi kuhakikisha kazi inakwenda kwa kasi, huku akibainisha kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutapunguza tatizo la mafuriko kwenye maeneo ya makazi.
Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, aliongeza msisitizo akisema kukamilika kwa barabara hiyo kutafungua fursa mpya za kiuchumi na kijamii katika jimbo hilo.
“Barabara hii ni uti wa mgongo wa shughuli za wananchi wetu—kuanzia usafirishaji wa mazao, kufika kwenye huduma za afya, hadi kukuza biashara ndogondogo. Tunashukuru Serikali kwa uwekezaji huu mkubwa, na tunawataka wakandarasi wahakikishe thamani ya fedha inaonekana,” alisema.
Aidha, Mbunge huyo alitumia nafasi hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa ofisi yake itaendelea kufuatilia maendeleo ya mradi huo kwa karibu ili kuhakikisha changamoto zozote zinazojitokeza zinapata ufumbuzi wa haraka.
Ends...




0 Comments