DC Mwinyi Awapa Madiwani Kazi Nzito: “Simamieni Fedha, Tatuleni Kero za Wananchi”
Na Joseph Ngilisho – ARUMERU
MKUU wa Wilaya ya Arumeru, Mwinyi Mwinyi, ametoa rai kwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC) kuhakikisha wanatekeleza ipasavyo majukumu yao ya kuwaletea wananchi maendeleo, ikiwemo kusimamia kikamilifu matumizi ya fedha za halmashauri hiyo.
Ametoa wito huo leo dec 2,2025 katika mkutano wa kwanza wa Baraza la Madiwani wa Arusha DC, ulioambatana na uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa halmashauri, ambapo madiwani kutoka kata 27 walipiga kura za ndiyo kuwapitisha viongozi hao.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwinyi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa madiwani katika kutekeleza majukumu yao, akibainisha kuwa uongozi ni utoaji wa huduma na si nafasi ya kujipatia hadhi.
> “Nendeni mkahudumie wananchi pale ambapo kiongozi anatakiwa. Usimame, ukae au hata ukimbie kwa ajili ya maslahi mapana ya wananchi—fanyeni hivyo,” alisema DC Mwinyi.
Pia aliwataka madiwani kutambua wajibu wao wa kuwa matumaini kwa wananchi, akisisitiza kuwa wakati mwingine viongozi wanapaswa kuwa watulivu na kutumia busara ili kulinda maslahi mapana ya jamii.
Katika kusisitiza umuhimu wa kusimamia maendeleo, Mwinyi aliweka wazi kuwa changamoto ya miundombinu, hususan barabara za ndani, bado ni kubwa. Kati ya takribani kilomita 796 za mtandao wa barabara katika halmashauri hiyo, ni kilomita 14 pekee zilizo katika kiwango cha lami, sawa na asilimia 1.8.
Alibainisha kuwa sehemu kubwa ya barabara hizo zipo katika kiwango cha changarawe, hali inayowapa madiwani wajibu mkubwa wa kujipanga na kujadili mikakati ya kupunguza changamoto hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Meru, Noel Severe, aliwataka madiwani na watumishi wa halmashauri kuimarisha umoja na mshikamano ili kutekeleza kwa ufanisi gurudumu la maendeleo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Johannes Lukumay, alisisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto sugu za maji na barabara, akibainisha kuwa wananchi wa maeneo ya Ngaramtoni, Oldonyosambu na maeneo mengine bado wanakabiliana na adha ya upatikanaji wa maji, huku nishati ya umeme nayo ikiendelea kuwa changamoto katika baadhi ya maeneo.
Ends..





0 Comments