Uzinduzi wa Kituo Kipya cha Mafuta cha AsamOil Ainon Watajwa Kuwa Chachu ya Maendeleo Arusha
Na Joseph Ngilisho – Arushadigital
Uzinduzi wa kituo kipya cha mafuta cha AsamOil kilichopo Kata ya Ainon, Jijini Arusha, umeendelea kuvutia hisia chanya za wananchi baada ya kutajwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa eneo hilo na Mkoa wa Arusha kwa ujumla. Uwekezaji huo umeongeza fursa za ajira, kuimarisha upatikanaji wa huduma za mafuta kwa karibu na kuchangia kwa kiasi kikubwa mzunguko wa uchumi wa jamii.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi, Mkurugenzi wa AsamOil, Ambrose Davie, aliwahakikishia wananchi upatikanaji wa mafuta safi, salama na yenye viwango vinavyokubalika kitaifa, akisisitiza kuwa dhamira ya kampuni ni kutoa huduma bora zitakazokidhi mahitaji ya wateja na kukuza ustawi wa jamii inayowazunguka.
“Kuanzia leo, Desemba 19, baada ya uzinduzi rasmi wa kituo hiki, wateja watapata punguzo maalum la hadi asilimia 80 kwa kila lita ya mafuta hadi mwisho wa mwaka huu,” alisema Davie, akibainisha kuwa kituo hicho ni cha 23 katika mtandao wa AsamOil nchini, huku maandalizi ya kufungua vituo vingine vipya Jijini Arusha yakiendelea.
Kwa upande wake, Meneja wa AsamOil, Leonard Mhina, alisema ufunguzi wa kituo hicho ni hatua muhimu katika kuchochea uchumi wa Mkoa wa Arusha, hususan kwa wananchi wanaotegemea sekta ya usafirishaji kama chanzo kikuu cha kipato.
Mhina aliwataka wananchi kutumia fursa ya huduma hiyo mpya kujiongezea kipato, akiwalenga zaidi waendesha bodaboda, ambao baadhi yao walipata fursa ya kujaziwa mafuta bure kama ishara ya kutambua mchango wao katika sekta ya usafirishaji wa abiria, pamoja na kuimarisha uhusiano kati ya kampuni na wateja wake wa mwanzo.
Mbali na huduma za mafuta, uzinduzi wa kituo hicho uliambatana na matendo ya kijamii, ambapo wamiliki wa kituo waligawa chakula na vinywaji kwa waendesha bodaboda, wananchi wa kawaida pamoja na watoto, kama sadaka na ishara ya shukrani, kuwathamini wateja na kushiriki furaha ya uzinduzi huo na jamii inayowazunguka.
Hatua hiyo ilipokelewa kwa furaha kubwa na wananchi, wengi wao wakieleza kuwa imeimarisha mahusiano kati ya mwekezaji na jamii, na kuonesha mfano wa uwekezaji wenye kugusa maisha ya watu moja kwa moja.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Wilfred Soilei, aliwapongeza wamiliki wa AsamOil kwa uamuzi wao wa kuwekeza Jijini Arusha, hususan katika maeneo yenye uhitaji mkubwa wa huduma ya mafuta, akieleza kuwa uwekezaji wa aina hiyo unachangia kukuza uchumi wa ndani na kupanua wigo wa ajira.
Soilei aliwahimiza wananchi kuunga mkono uwekezaji huo kwa kutumia mafuta ya kituo hicho, huku akiwataka wahudumu kuhakikisha wanatoa huduma zenye weledi, uadilifu na heshima ili kujenga imani ya wateja na kudumisha hadhi ya kampuni.
Uzinduzi wa kituo cha AsamOil Ainon umeacha alama chanya kwa wakazi wa Arusha, ukionesha kuwa uwekezaji wa kisasa unaweza kwenda sambamba na uwajibikaji wa kijamii, hivyo kuwa nguzo muhimu ya maendeleo endelevu ya jamii na taifa kwa ujumla.













0 Comments