RC MAKALLA AIPA JIJI LA ARUSHA DIRA MPYA YA MAPATO, HUDUMA NA MAENDELEO
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
MAPATO ni uti wa mgongo wa maendeleo na bila kuyasimamia ipasavyo, Halmashauri haiwezi kujenga uwezo wa kuwahudumia wananchi kwa ufanisi. Kauli hiyo nzito imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, alipolihutubia Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Arusha, akisisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa vyanzo vya mapato ndio msingi wa utoaji bora wa huduma kwa jamii.
Akizungumza leo Jumanne, Desemba 16, 2025, katika kikao cha Baraza la Madiwani, Makalla ameliagiza Baraza hilo kuweka mikakati madhubuti ya kukusanya na kusimamia mapato, sambamba na kuboresha huduma katika vyanzo hivyo, hususan masoko, akieleza kuwa takwimu za ukusanyaji mapato kwa sasa bado haziridhishi.
Amesisitiza kuwa wajibu wa Madiwani hauishii kwenye ukusanyaji pekee, bali pia kwenye kuhakikisha vyanzo vya mapato vinasimamiwa kwa weledi, uwazi na ufanisi, huku akiwataka kufanya kazi kwa umoja, mshikamano na kwa kuwatumia ipasavyo wataalamu wa Halmashauri katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amewataka Madiwani hao kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao, akisisitiza kuwa miradi yote ikamilike kwa wakati na kwa viwango vilivyokubaliwa katika mikataba. Miradi hiyo ni pamoja na Kituo Kikuu cha Mabasi, Soko la Kilombero, Uwanja wa Michezo wa Bondeni City na Jengo la Utawala la Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Akizungumza kwa niaba ya Baraza la Madiwani, Diwani wa Kata ya LEVOLOS , ABBAS HAJ, amesema maelekezo ya Mkuu wa Mkoa yamekuja wakati muafaka na yamewapa Madiwani mwelekeo mpya wa kuimarisha uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Amesema Baraza la Madiwani limejipanga kuyafanyia kazi maelekezo hayo kwa vitendo kwa kushirikiana na wataalamu wa Halmashauri, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha kila chanzo cha mapato kinatoa mchango stahiki na miradi yote inatekelezwa kwa ubora unaotarajiwa.
Kwa upande wake, Makalla pia ameelekeza kupewa kipaumbele suala la usafi wa mazingira ili Jiji la Arusha liendane na hadhi yake ya kitovu cha utalii, sambamba na kuhimiza ukuzaji wa utalii wa michezo kama fursa ya kiuchumi. Aidha, amesisitiza uwazi na usimamizi makini katika utoaji wa mikopo ya asilimia kumi kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Kwa kumalizia, Mkuu wa Mkoa amewahimiza Madiwani kuwa karibu na wananchi, kusikiliza kero zao na kuzitatua kwa wakati, akisisitiza kuwa uongozi unaopimika ni ule unaogusa maisha ya wananchi na kuleta matokeo chanya ya maendeleo kwa jamii nzima.
-ends..




0 Comments