MSUMARI WA RC MAKALA KWA BODABODA NA BAJAJI ARUSHA ATOA MAELEKEZO MAZITO KWA WAKUU WA WILAYA,AMPA SIKU SABA DC MKUDE WA ARUSHA

RC MAKALLA ATUMA UJUMBE MZITO BAJAJI, BODABODA ARUSHA

Aunda kamati kupanga vituo na njia mpya, atoa siku saba kutatua mgogoro wa uongozi
Aagiza polisi kukomesha uhalifu wa ‘Tatu Mzuka’

Na Joseph Ngilisho-Arusha


MKUU wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos  Makalla, ameagiza kufanyika kwa maboresho ya haraka ya vituo na njia rasmi za Bajaji na Bodaboda ndani ya Jiji la Arusha, akisisitiza kuwa usafiri huo ni chanzo halali cha kipato lakini lazima usimamiwe kwa nidhamu, mpangilio na haki kwa wadau wote wa barabara.

Akizungumza leo Jumatatu Desemba 15, 2025 katika viwanja vya Makumbusho ya Azimio jijini Arusha wakati wa zoezi la kusikiliza na kutatua kero za waendesha pikipiki na bajaji,  Makalla ametangaza kuundwa kwa kamati maalumu itakayowahusisha wadau wa usafiri, serikali za mitaa na vyombo vya usalama kwa lengo la kupitia upya vituo na barabara zitakazotumika na vyombo hivyo.

Alisema lengo la hatua hiyo ni kuondoa msongamano, migogoro ya mara kwa mara baina ya bajaji, bodaboda na madereva wa daladala, pamoja na kuimarisha usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara.

> “Ni wakati sahihi sasa bajaji na bodaboda wapangiwe vituo rasmi na njia zao bila kuathiri wadau wengine. Wote hawa wanatafuta riziki, na ni wajibu wa serikali kusimamia ili kila mmoja afanye kazi kwa amani na utulivu,” alisema Makalla.





Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amempa siku saba Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Modest Mkude, kushughulikia kwa uzito mgogoro wa uongozi unaokikumba chama cha bodaboda mkoani Arusha kwa ngazi ya wilaya na Mkoa.

Mgogoro huo unahusisha malalamiko ya uongozi, umiliki wa fedha na kutokuwepo kwa mwafaka miongoni mwa wanachama, ikiwemo mvutano juu ya mpango wa kujisajili kama chama cha ushirika.

> “Natoa siku saba kwa DC Arusha akutane na uongozi wa bodaboda wa wilaya na mkoa, wakae mezani, wajadiliane kwa uwazi na kupata suluhisho la kudumu. Serikali haitavumilia migogoro inayoathiri amani na shughuli za vijana,” aliagiza Makalla.


Aidha, Makalla ametoa onyo kali kwa waendesha pikipiki wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu wanaojulikana kama ‘Tatu Mzuka’, akieleza kuwa kundi hilo limekuwa tishio kwa usalama wa wananchi kwa kuwabeba watu watatu na kuwaporwa watembea kwa miguu.

Kutokana na hali hiyo, ameagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kuchukua hatua za haraka na kali kukomesha uhalifu huo.

> “Niwatahadharishe wanaotumia pikipiki kuiba wananchi, hasa hawa ‘Tatu Mzuka’. Waache mara moja, watafute kazi halali za kufanya. Polisi wachukue hatua bila kusita,” amesisitiza.


Sambamba na hayo, Mkuu wa Mkoa amewaelekeza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zote mkoani Arusha kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu mikopo ya halmashauri inayotolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, akibainisha kuwa bado kuna upungufu mkubwa wa taarifa na uelewa miongoni mwa walengwa.

Alisema serikali imeweka fedha hizo kwa nia njema ya kuinua uchumi wa wananchi, hivyo ni wajibu wa viongozi kuhakikisha taarifa sahihi zinafika kwa wananchi na mikopo hiyo inawanufaisha walengwa waliokusudiwa.

--ends..

Post a Comment

0 Comments