Wizara ya Fedha Yataka Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Kuzingatia Dira ya Taifa ya 2050 Kuimarisha Utawala Bora
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
WIZARA ya Fedha imewataka wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, hatua inayolenga kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.
Wito huo umetolewa leo Desemba 19,2025 na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, kwa niaba ya Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Munde, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 16 wa Mwaka wa Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi unaosimamiwa na Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), uliofanyika jijini Arusha.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Omar alisema kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 kunategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa wataalamu wenye sifa, uadilifu na wanaotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na mifumo iliyopo.
Alifafanua kuwa Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa ununuzi na ugavi kwa kuunganisha mfumo wa usajili wa wataalamu wa PSPTB na Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Kielektroniki (NeST), ili kuhakikisha wanaotekeleza majukumu hayo wanakuwa na sifa stahiki na kutambulika kisheria.
“Hakuna maendeleo ya kweli yanayoweza kupatikana bila mifumo madhubuti ya ununuzi na ugavi. Ndiyo maana Serikali imeweka mkazo kwenye matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kuongeza uwazi, ufanisi na kuzuia mianya ya ubadhirifu,” alisema Balozi Omar.
Hata hivyo, alitoa onyo kali kwa watu wanaotekeleza shughuli za ununuzi na ugavi bila kuwa na sifa stahiki, hususan katika mamlaka za serikali za mitaa, akisisitiza kuwa kitendo hicho ni ukiukwaji wa Sheria ya Ununuzi na Ugavi na hakitavumiliwa.
Katika hatua nyingine, aliihimiza sekta binafsi kuzingatia kikamilifu sheria, kanuni na taratibu za ununuzi na ugavi katika utekelezaji wa shughuli zao, akisema kuwa sekta hiyo ni mdau muhimu katika kufanikisha ajenda ya maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PSPTB, Jacob Kibona, alisema bodi hiyo imepata mafanikio makubwa ikiwemo kusimamia na kuendeleza mitaala ya kitaaluma inayolenga kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, maarifa na maadili ya taaluma ya ununuzi na ugavi.
Aliongeza kuwa PSPTB pia imefanikiwa kutoa mafunzo endelevu ya maendeleo ya kitaaluma (CPD) kwa wataalamu, sambamba na kuboresha matumizi ya mifumo ya kidijitali, hususan mfumo wa usajili, hatua inayochangia kuongeza ufanisi na uwazi katika sekta hiyo.
Mkutano huo wa mwaka umezikutanisha taasisi za umma na binafsi, wataalamu na wadau wa sekta ya ununuzi na ugavi kwa lengo la kujadili namna bora ya kuimarisha taaluma hiyo katika kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Ends..




0 Comments