MBUNGE LUKUMAY AREJESHA MAJI NDANI YA SIKU TATU YALIYOKATWA MUDA MREFU KWA DENI LA 780,000 SHULE YA MUUNGANO , WANANCHI WAMSHANGILIA AONEKANA SHUJAA,DIWANI MREMA NAYE ALAMBA DUME

 MBUNGE LUKUMAY AREJESHA MAJI SHULE YA MUUNGANO NDANI YA SIKU TATU, WANAFUNZI 1,500 WAPUMUA

Na Joseph Ngilisho – ARUMERU

MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, amefanikiwa kutatua changamoto ya maji katika Shule ya Msingi Muungano iliyopo Kiserian, Kata ya Mlangarini mkoani Arusha, ndani ya siku tatu tu baada ya huduma hiyo kusitishwa kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na deni la ankara ya maji la Sh 780,000.

Huduma ya maji katika shule hiyo ilikuwa imekatwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) kutokana na malimbikizo ya deni, hali iliyosababisha adha kubwa kwa wanafunzi zaidi ya 1,500 waliokuwa wakilazimika kutumia muda mwingi kutafuta maji mitaani badala ya kusoma, huku wengine wakikosa huduma za msingi za usafi ikiwemo vyoo.

Akizungumza leo desemba 20,2025 mbele ya wananchi na viongozi wa kata hiyo, Dkt. Lukumay alisema alipata taarifa ya kero hiyo alipofika Mlangarini kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kumchagua na kusikiliza kero zao.

 Alisema aliichukulia changamoto hiyo kwa uzito na kuanza mara moja kufuatilia hadi kufanikisha kurejeshwa kwa huduma ya maji ndani ya siku tatu.

“Nilipofika hapa viongozi wa kijiji walinieleza kuhusu maji kukatwa katika shule hii. Nilichukua hatua za haraka, nikafuatilia na leo nimefika kuwaeleza wananchi kuwa tatizo limepatiwa ufumbuzi. Wanafunzi sasa watasoma bila usumbufu wa kutafuta maji,” alisema Dkt. Lukumay.

Aliishukuru AUWSA kwa usikivu na ushirikiano waliouonesha kwa kurejesha huduma hiyo muhimu, hususan katika maeneo yenye uhitaji wa haraka kama shule. Aidha, aliwahimiza wananchi na wakazi wa eneo hilo kulipa ankara za maji kwa wakati ili kuziwezesha mamlaka husika kujiendesha na kusambaza huduma kwa ufanisi.

Dkt. Lukumay alishangiliwa na wananchi waliokusanyika kushuhudia maji yakianza kutoka tena shuleni hapo, wakionesha furaha yao licha ya mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.

 Mbunge huyo aliahidi kuendelea kushughulikia kero mbalimbali za wananchi bila kuchoka na kuhakikisha wanapata huduma muhimu za kijamii kwa wakati. Pia aliwataka watendaji na madiwani kuwa karibu na wananchi na kutatua changamoto zao kwa haraka.


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mlangarini, Emmanuel Mrema, alimshukuru Mbunge Lukumay kwa kuonesha uchapakazi na moyo wa kizalendo kwa kurejesha huduma ya maji katika kata hiyo baada ya kipindi kigumu kwa wazazi, walimu na wanafunzi.

“Ndani ya siku mbili baada ya mbunge kufika shuleni na kukutana na kero hii, aliichukua kwa uzito. Leo maji yamepatikana licha ya kukatwa awali kutokana na usimamizi mbovu uliosababisha malimbikizo ya deni,” alisema Mrema.

Alimhakikishia mbunge kuwa hatua madhubuti zitachukuliwa kuhakikisha usimamizi mzuri wa huduma ya maji shuleni hapo ili kuepuka kurejea kwa tatizo hilo, akisisitiza kuwa mazingira bora ya kujifunzia yatachangia kuboresha ufaulu wa wanafunzi waliokuwa wakipoteza masomo kwa kutafuta maji.

Naye mwananchi, Miriamu Kivuyo, alisema awali shule hiyo ilikuwa ikifanya vizuri kitaaluma lakini ilianza kuporomoka kutokana na wanafunzi kutumia muda mwingi kutafuta maji. Alidai kuwa licha ya wananchi kuchangia fedha kwa ajili ya huduma ya maji, uongozi wa shule haukuwa ukiwasilisha fedha hizo ipasavyo hali iliyosababisha deni kukua.

Aliongeza kuwa hata baada ya wafadhili kusaidia kujenga matenki ya kuvuna maji ya mvua na shule kuwekwa matirizi, changamoto ya maji iliendelea kuwa kubwa, hali iliyowaathiri wanafunzi katika usafi wa madarasa na matumizi ya vyoo. Alimpongeza Dkt. Lukumay kwa hatua za haraka na kuonesha kuwa amekuwa mstari wa mbele kutatua kero za wananchi.

Katibu wa Siasa na Uenezi  (ccm) Arumeru, Nicholus Sawa, aliitaka AUWSA kuepuka kukata maji katika maeneo ya umma kama shule, akisema hatua hiyo hunyima wanafunzi haki ya msingi ya kupata mazingira salama ya kujifunzia.

 Alipendekeza mamlaka hiyo kutumia majadiliano na kupanga utaratibu wa ulipaji wa madeni badala ya kusitisha huduma na kuondoa mita za maji.

Akizungumza kwa niaba ya AUWSA, Afisa Uhusiano, Mary Jackson, alisema changamoto hiyo ni ya kawaida na ilitatuliwa kwa wakati. Aliwasihi wananchi kuwa na utaratibu wa kulipa ankara zao kwa wakati ili kuepuka usumbufu, akisisitiza kuwa kila mtumiaji wa maji ya AUWSA—iwe ni taasisi ya umma, kampuni binafsi au mtu mmoja mmoja—ana wajibu wa kulipa bili ya maji.

“Tunawasihi wananchi wawajibike kulipa bili zao kwa wakati. Mtu anapochelewa miezi miwili au mitatu, deni huongezeka na hatimaye husababisha kukatiwa huduma,” alisema Jackson.






Ends...

Post a Comment

0 Comments