Majibu ya Upotoshaji Kuhusu Maendeleo ya Tanzania
By Arushadigital
Tarehe 5 Desemba, Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uswidi, Bw. Benjamin Dousa, alitangaza uamuzi wa Serikali ya Uswidi kusitisha misaada ya maendeleo kwa nchi tano ambazo ni Tanzania, Msumbiji, Zimbabwe, Liberia na Bolivia, kufuatia mapitio ya vipaumbele vya sera za mambo ya nje pamoja na changamoto za kiusalama.
Hata hivyo, katika tangazo hilo, kulijitokeza kauli iliyozua mjadala mpana baada ya nchi hizo kutajwa kuwa “zimekwama katika ujamaa” na “kushindwa kupiga hatua za maendeleo.” Kauli hiyo ilizua tafsiri potofu kuhusu historia, mwelekeo na mafanikio ya kiuchumi ya Tanzania.
Kupitia makala iliyochapishwa tarehe 16 Desemba 2025 katika gazeti la Aftonbladet nchini Uswidi, Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Mobhare Matinyi, anatoa majibu ya kina akielezea safari ya maendeleo ya Tanzania kwa zaidi ya miongo sita.
Historia ya Ushirikiano wa Tanzania na Uswidi
Serikali ya Uswidi ilitangaza kuwa itasitisha misaada yake ya ushirikiano wa maendeleo kwa nchi tano kabla ya mwisho wa mwaka 2026, hatua inayohitimisha uhusiano wa misaada uliodumu kwa miongo kadhaa.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa, licha ya kuwa imekuwa na uhusiano wa karibu na Uswidi kwa zaidi ya miaka 62. Uhusiano huu ulijengwa juu ya misingi ya itikadi zinazofanana za demokrasia ya kijamii, falsafa inayosisitiza haki ya kijamii, usawa, utu wa binadamu na mshikamano wa kijamii, huku serikali ikichukua nafasi ya kurekebisha athari za soko huria.
Wakati Uswidi iliendesha demokrasia ya vyama vingi ndani ya uchumi wa kibepari wenye ustawi, Tanzania ilichagua mfumo wa chama kimoja uliotawaliwa na Ujamaa wa Kiafrika, uliolenga kujitegemea na usawa wa kijamii. Katika muktadha huo, Uswidi ilichukua nafasi ya kuisaidia Tanzania kujenga harakati za vyama vya ushirika kama nyenzo ya maendeleo.
Tofauti za Awali za Kiuchumi
Mwanzoni mwa miaka ya 1960, tofauti za kiuchumi kati ya nchi hizi mbili zilikuwa dhahiri. Mwaka 1961, Uswidi ikiwa na watu milioni 7.5 ilikuwa na Pato la Taifa la dola bilioni 17.33, ikitegemea uchumi wa viwanda. Tanzania, yenye watu milioni 10.3, ilikuwa na Pato la Taifa la dola bilioni 2.83 na uchumi uliotegemea zaidi kilimo.
Kutokana na dira ya maendeleo iliyooneshwa na Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Julius Nyerere, Uswidi iliona umuhimu wa kuiunga mkono Tanganyika mwaka 1963, kabla ya muungano na Zanzibar mwaka 1964.
Simulizi Potofu na Ukweli wa Maendeleo
Kauli ya hivi karibuni ya Serikali ya Uswidi ilijenga taswira isiyoakisi uhalisia, kwa kudai kuwa nchi husika “zimekuwa zikifuata ujamaa kwa muda mrefu na hazijaendelea.” Kwa Tanzania, kauli hiyo ni upotoshaji wa wazi.
Elimu ya Juu
Mwanzoni mwa miaka ya 1960, Tanzania ilikuwa na chuo kikuu kishiriki kimoja pekee. Leo, nchi ina vyuo vikuu 36 vilivyosajiliwa na vyuo vikuu vishiriki 16. Kwa kulinganisha, Uswidi ina vyuo vikuu 18 na vishiriki 12. Kwa idadi ya watu takribani milioni 70, Tanzania bado ina mahitaji makubwa zaidi ya miundombinu ya elimu ya juu.
Sekta ya Afya
Miaka ya awali, Tanzania ilikuwa na vituo 1,343 vya kutolea huduma za afya, vikiwemo hospitali 96. Leo, idadi hiyo imeongezeka hadi vituo 13,606, vikiwemo hospitali 473 na vituo vya afya 1,348. Ushirikiano wa muda mrefu kati ya Hospitali ya Karolinska ya Stockholm na Hospitali ya Taifa Muhimbili ni ushahidi wa mafanikio ya ushirikiano huu.
Miundombinu na Usafirishaji
Tanzania ilianza na uwanja mmoja wa ndege wa kimataifa Dar es Salaam, lakini sasa ina viwanja vya Kimataifa vya Kilimanjaro na Zanzibar, huku Dodoma na Mwanza vikiendelea kuboreshwa.
Bandari nne kuu za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Zanzibar, pamoja na bandari za maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa, zinaifanya Tanzania kuwa lango muhimu kwa nchi zisizo na bandari Afrika Mashariki. Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo unatarajiwa kuimarisha nafasi hiyo.
Mtandao wa barabara na reli, ukiwemo mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaotumia umeme — wa kwanza Afrika Mashariki na Kati — ni uthibitisho wa kasi ya maendeleo ya miundombinu.
Nishati na Uchumi wa Baadaye
Tanzania inajiandaa kuwa kitovu cha nishati baada ya kukamilika kwa mradi wa gesi asilia wa dola bilioni 42 unaoshirikisha kampuni ya Equinor ya Norway. Aidha, Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki kutoka Uganda hadi Tanga linakaribia kukamilika.
Kwa upande wa umeme, Tanzania inazalisha maelfu ya megawati kupitia nguvu za maji na inawekeza katika jotoardhi, upepo na nishati ya jua, sambamba na akiba kubwa ya makaa ya mawe inayokadiriwa kufikia tani bilioni 1.9.
Ukuaji wa Uchumi na Biashara
Pato la Taifa la Tanzania linakaribia dola bilioni 90, huku ukuaji wa uchumi ukiwa kati ya asilimia 5–7 kwa mwaka tangu 2000, kwa mujibu wa Benki ya Dunia na Shirika la Mikopo ya Mauzo ya Nje la Uswidi (EKN). Mwaka 2020, Tanzania ilipandishwa hadhi na kuwa nchi ya kipato cha kati.
Mwelekeo wa sasa ni kutoka misaada kwenda biashara na uwekezaji, hali inayoifanya Tanzania kuikaribisha sekta binafsi ya Uswidi kuwekeza katika viwanda, madini, utalii, kilimo na teknolojia.
Utalii, Madini na Uwekezaji
Katika mwaka unaoishia Septemba 2025, Tanzania ilipata dola bilioni 4.43 kutokana na mauzo ya dhahabu nje ya nchi, huku utalii ukitarajiwa kuingiza dola bilioni 6.0 ifikapo mwisho wa 2025. Tanzania imeendelea kuongoza duniani kwa utalii wa mbugani kwa mwaka wa tatu mfululizo.
Aidha, nchi inashika nafasi ya tatu Afrika na ya sita duniani kwa akiba ya madini muhimu. Mwaka 2024 pekee, Tanzania ilivutia uwekezaji wa moja kwa moja wa dola bilioni 9.31 kupitia miradi 901 iliyosajiliwa, na inajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 140.
Hitimisho
Chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania inaendelea kutekeleza mikakati madhubuti ya maendeleo jumuishi na endelevu. Kwa uchumi unaofuata soko huria, wenye sekta nyingi na ukuaji thabiti, kuitaja Tanzania kama nchi “iliyokwama katika ujamaa usio na maendeleo” si sahihi bali ni upotoshaji wa wazi wa ukweli.
Mwandishi ni Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nchi za Nordic, Baltic na Ukraine, mwenye makazi yake Stockholm.
Ends..


0 Comments