TEC: Maandamano Ni Haki Ya Raia, Adhabu Si Kifo – Askofu Pisa Ataka Uwajibikaji
By Arushadigtal, Dar es Salaam
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kupitia kwa Rais wake ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Mhashamu Wolfgang Pisa, limeeleza kuwa maandamano ni haki ya msingi ya raia ikiwa ni njia ya kufikisha ujumbe au malalamiko pale majadiliano yanaposhindikana. Hata hivyo, limesisitiza kuwa maandamano hayo yafanyike kwa amani na uadilifu, na siyo kwa matumizi ya nguvu au vurugu.
Akizungumza kupitia taarifa ya TEC, Askofu Pisa amesema ni jambo la kusikitisha kuona waandamanaji wote waliotokea siku ya uchaguzi kuonyeshwa kama wahalifu, na hata baadhi kufungiwa katika mwamvuli wa uhalifu bila kosa lililoainishwa kisheria.
> “Adhabu ya mwandamanaji siyo kuuawa. Kila mtu anayo haki ya kuishi, na jamii ina wajibu wa kulinda uhai huo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 14,” alisisitiza.
Uvunjiwaji wa Haki za Binadamu
TEC imeeleza kuwa maandamano hayo yamechochewa na matukio ya wazi ya uvunjaji wa haki za binadamu ikiwemo mauaji, utekaji, kujeruhi na utesaji wa raia bila hatua stahiki kuchukuliwa. Aidha, imesema matukio hayo yanakiuka sio tu Katiba, bali pia misingi ya utu na heshima ya binadamu.
> “Haki hii imethibitishwa kukiukwa na vyombo vya ulinzi au ‘wasiojulikana’ ambao wanaonekana kuwa na nguvu kuliko dola yenyewe,” aliongeza Askofu Pisa.
ICE: Demokrasia ya Kweli Inahitajika
Akigusia chanzo kingine cha maandamano, TEC imesema kukosekana kwa misingi ya demokrasia ya kweli katika chaguzi ni moja ya chachu ya machafuko hayo.
> “Tangu mwaka 2016, tumekuwa na kilio cha muda mrefu kuhusu upatikanaji wa viongozi kwa njia ya haki, uwazi, ushindani wa kweli na uhuru. Hadi leo hakijapatiwa ufumbuzi,” ilieleza taarifa ya Baraza.
Vyombo vya Usalama Valaumiwa
Baraza hilo pia limekosoa namna vyombo vya usalama vilivyojiepusha kutumia mbinu za kijeshi katika kudhibiti maandamano, likionyesha kuwa matumizi ya silaha za moto hayakuwa ya lazima.
> “Hata katika vita, zipo silaha zinazokatazwa. Lakini katika maandamano ya amani, tumeshuhudia matumizi ya risasi za moto, jambo ambalo ni kinyume na mwongozo wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1990 kuhusu matumizi ya nguvu,” limesema TEC.
TEC imetaka uchunguzi wa kina na uwazi kuhusu vifo vilivyotokea, ikisisitiza kuwa askari walioua raia wasio na silaha lazima wawajibishwe.
> “Askari waliua ndugu zetu wasio na silaha holela na kwa ukatili mkubwa kama wanyama. Binadamu mwenye akili timamu anawezaje kufanya vitendo kama hivyo?” alihoji Askofu Pisa.
Akihitimisha, TEC imewataka viongozi na vyombo vya dola kuweka maslahi ya taifa mbele, kuzingatia sheria, na kulinda haki za kila mwananchi bila upendeleo.
#Arushadigital Update

0 Comments