SAMIA AAGIZA KUACHIWA KWA VIJANA WALIOSHTAKIWA KWA MAKOSA YA UHAINI

Rais Samia Aagiza Uchujaji wa Mashitaka Dhidi ya Vijana Walioshtakiwa kwa Uhaini

By Arushadigital -DODOMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameielekeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuchuja kwa umakini mashitaka yanayowakabili vijana waliokamatwa kufuatia maandamano ya Oktoba 29, 2025, hususan wale waliobainika kushiriki bila kujua madhara ya kitendo chao.



Akihutubia Bunge leo, Novemba 14, 2025, Rais Samia alisema kundi kubwa la vijana waliojipata humo katika maandamano walifuata “mkumbo” bila dhamira ya kufanya makosa ya jinai au kuhatarisha usalama wa nchi.

> “Natambua kuna vijana wengi waliokamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini. Wengine hawakujua wanachokifanya, wengine walifuata mkumbo. Nikiwa kama mama, navielekeza vyombo vya kisheria kuangalia upya makosa yaliyofanywa na vijana wetu,” alisema Rais Samia.


Ameelekeza kuwa vijana ambao hawakudhamiria kufanya uhalifu, na ambao ushahidi unaonyesha walijikuta kwenye maandamano kwa ushabiki au kufuata makundi, waachiwe huru na kurejeshwa kwa wazazi wao ili kuendelea na maisha yao.

> “Ukiangalia clip za maandamano unaona kabisa kuna vijana waliingia kwa kufuata mkumbo, wanaimba kwa ushabiki. Naelekeza Ofisi ya DPP kuchuja viwango vya makosa, na kwa wale waliosukumwa na mkumbo tu—waachiwe waende kwa wazazi wao,” alisisitiza.


Kauli ya Rais Samia imeonekana kuwa ujumbe mzito kwa vyombo vya dola, ikilenga kulinda haki za vijana, kupunguza mzigo wa mashitaka ya jumla, na kuhakikisha adhabu inatolewa tu pale panapothibitishwa dhamira ya kweli ya kuvunja sheria.

Wachambuzi wa masuala ya haki na utawala bora wanasema hatua hiyo inaweza kuleta maridhiano na kuleta taswira mpya ya kisheria katika kushughulikia makosa yanayohusisha makundi ya vijana nchini.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments