Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
Viongozi Shura ya Maimamu -ArushaSHURA ya Maimamu na Viongozi wa Taasisi za Kiislamu Arusha ,imetoa tamko kali la kulaani machafuko ya uchaguzi wa Oktoba 29, mwaka huu, na kutaka hatua madhubuti zichukuliwe kurejesha na kulinda amani ya nchi.
Sheikh Ikusi alisisitiza kuwa Tume Huru ya Uchunguzi iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan inapaswa kuja na majibu ya kweli, ya kina na yatakayoponya majeraha yaliyosababishwa na tukio hilo, ili kuepusha kurudiwa kwa machafuko nchini.
Katika tamko hilo, Sheikh Ikusi alionyesha kukerwa na baadhi ya matamko yaliyotolewa na viongozi wa Kikristo kupitia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), akidai kuwa yaliweza kuchochea mazingira ya vurugu wakati wa uchaguzi.
Shura ya Maimamu ilisisitiza kuunga mkono hatua ya Rais Samia ya kuunda Tume Huru ya Uchunguzi, wakisema ni hatua sahihi ya kupata ukweli, kujenga maridhiano na kurejesha mshikamano wa taifa.
Yataka uchunguzi wa kina kwenye chanzo cha machafuko
Tamko hilo limeitaka tume hiyo kuchunguza masuala muhimu, ikiwemo,Nani au kikundi gani kilichochochea machafuko na kusababisha uharibifu wa mali na vifo.Mapungufu ya serikali au mifumo ya usimamizi wa uchaguzi.
Sheikh Ikusi aliitahadharisha jamii dhidi ya kauli za uchochezi zinazosambaa mtandaoni zinazodaiwa kutolewa na watu wanaojiita Waislamu, akisema hizo si fundisho la dini na zinapaswa kupuuzwa.
> “Tusipowakemea watu hawa, taifa letu linaweza kuingia katika hali ya machafuko kama baadhi ya nchi jirani ambako vurugu zimekuwa zikijirudia bila kikomo,” alisema.
Viongozi wa dini waliohudhuria tamko hilo, akiwemo Sheikh Suleiman Mgulumah na Sheikh Farajallah Soly, waliwahimiza Watanzania kuendelea kuilinda amani, wakiitaja kuwa ndiyo msingi wa maendeleo na ustawi wa taifa.
Ends









0 Comments